Akitoa salamu za Bunge kupitia kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu, utamaduni na michezo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Husna Sekiboko, ameiomba serikali kuharakisha utoaji wa bajeti kwaajili ya utekelezaji wa ujenzi wa vyuo 64 vya ufundi stadi nchini ili kutoa fursa ya vijana kupata ujuzi mbalimbali na kuondokana na changamoto ya ajira iliyopo nchini.

Mhe. Sekiboko ametoa ombi hilo mapema leo Jumanne Machi 18, 2025, wakati wa ufunguzi wa kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya VETA, hafla inayoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye kituo cha kimataifa cha mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar Es salaam.
Mhe. Sekiboko ametoa pongezi pia kwa serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa ya sekta ya elimu ya ufundi stadi nchini, akieleza kuwa ujenzi wa vyuo vya Veta kwenye wilaya zote nchini sambamba na ujenzi wa Karakana za kujifunzia na kufundishia kumetoa mchango mkubwa katika upunguzaji wa tatizo la ajira kwa vijana.

Akizungumzia umuhimu wa elimu ya Ufundi, Mhe. Sekiboko amesema alipomaliza elimu yake ya chuo kikuu (degree ya ualimu) alirudi kusoma masomo ya Veta, akijifunza ushonaji wa viatu, suala ambalo lilimfanya kutimiza ndoto yake ya kuwa na kiwanda cha ushonaji wa viatu, viatu ambavyo ameeleza kuwa vimevaliwa hii leo na watu mbalimbali akiwemo Waziri wa viwanda na biashara Mhe. Seleman Jaffo na Mwanasiasa Mhe. Anastazia Wambura, kando ya Viongozi wengine kadhaa aliowataja ukumbini hapo.