Serikali ya Mapinduzi Visiwani Zanzibar imeeleza kuwa tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia Visiwani humo mnamo Mei 2023, tayari imetekelezwa kwenye mikoa miwili ya Mjini Magharibi na Kaskazini Pemba ambapo jumla ya wananchi 1246 wamefikiwa moja kwa moja kwa kupata msaada huo wa kisheria bure pamoja na elimu ya sheria, utawala bora na haki za binadamu.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumatano Aprili 23, 2025 na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, utumishi na Utawala bora visiwani Zanzibar Mansura Mosi Kassim, wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo kwenye Mkoa wa tatu wa Kaskazini Unguja, akimshukuru muasisi wa kampeni hiyo Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwa miongozo na maelekezo yao mbalimbali katika utekelezaji wa kampeni hiyo muhimu kwa wananchi hasa wale wasio na uwezo wa kugharamia huduma za kisheria.

Akizungumzia lengo la kampeni hiyo ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia, Mansura ameeleza kuwa lengo lake hasa ni kuimarisha upatikanaji wa haki na utoaji wa msaada wa kisheria na kuongeza uelewa wa haki za binadamu, kuimarisha utoaji wa huduma za ushauri wa kisheria na nasaha kwa waathirika na manusura wa ukatili wa kijinsia pamoja na kukuza uelewa kuhusu sheria, haki, wajibu na misingi ya utawala bora kwa wananchi na watendaji wa ngazi mbalimbali za jamii.

Ametumia fursa hiyo pia kutoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kujitokeza kwa wingi kwenye siku zote tisa za utekelezaji wa kampeni hiyo kwenye mkoa huo, akiwataka wenye kero na malalamiko mbalimbali kuyawasilisha kwa wanasheria wanaotekeleza kampeni hiyo iliyoasisiwa na kufadhiliwa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mgeni Rasmi katika Kampeni hiyo inayoratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria ya Tanzania bara na ile ya Zanzibar ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Visiwani Zanzibar Mhe. Dkt. Mwl. Haroun Ali Suleiman.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *