ACT Wazalendo tunaitaka Wizara ya Afya ya Tanzania, kueleza ukweli kuhusu mlipuko wa ugonjwa hatari wa Marbug, na itangaze hatua za tahadhari kuzuia kuenea ugonjwa huo Mkoani Kagera.
Kufuatia taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Dunia (WHO) Dkt. Tedros Ghebriyesus tarehe 15 Januari ambazo pia zilichapishwa kwenye tovuti rasmi ya WHO, tayari imezitaarifu nchi wanachama 194 kuhusu taarifa hii kuwa Mkoani Kagera kuna visa kadhaa vinavyohisiwa kuwa ni visa vya ugonjwa wa Marbug na kwamba watu 9 wamethibitika na watu 8 tayari wamefariki.
Taarifa hii ya WHO inakuja siku mbili baada ya ukurasa rasmi wa X wa Wizara ya Afya Tanzania kukanusha taarifa iliyoeleza uwepo wa ugonjwa huo Januari 13, 2025 na kuandika kuwa si taarifa ya kweli (FAKE) bila kuweka maelezo yoyote. Hata hivyo tarehe 15 Januari 2025, wizara ilikanusha taarifa za uwepo wa ugonjwa huo na kwamba imetuma wataalamu na sampuli zote zilizochukuliwa hazijaleta majibu ya uwepo wa ugonjwa huo.
Ugonjwa wa Marbug ni ugonjwa hatari sana, ambao mpaka sasa hauna tiba unaoambukizwa kwa damu, majimaji na kugusana, ugonjwa huu hatari unatoka jamii moja na kirusi kinachosababisha homa ya Ebola na una uwezekano wa kusababisha kifo kwa asilimia 88 kwa muathirika.
Taarifa ya Wizara ya jana usiku kukanusha uwepo wa ugonjwa huu bila tahadhari mpaka kushinikizwa na jumuiya ya kimataifa kunaacha maswali mengi na kunaiweka Tanzania mahali pabaya kimataifa, kunaishushia hadhi yake kubwa iliyojijengea hivi karibuni baada ya kushinda kiti cha ukurugenzi mkuu wa WHO kanda ya Afrika, pia kinadhihirisha ukweli kuwa Wizara ya Afya haijali usalama wa wananchi kwa kukaa kimya muda mrefu licha ya kuwepo viashiria vya ugonjwa huo.
ACT Wazalendo tunaitaka Wizara ya Afya ieleze umma ukweli, wagonjwa waliochukuliwa sampuli kama taarifa yao inavyodai wamegundulika na ugonjwa gani wenye dalili sawa na Marburg, wizara ieleze watu 8 wanaotajwa na WHO kufariki kwa ugonjwa huo wamefariki kwa ugonjwa gani ikiwa wanakanusha.
Aidha tunaitaka Wizara ya Afya itangaze haraka hatua za tahadhari kwa umma juu ya namna ya kujikinga na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo hatari na kufanya uchunguzi zaidi kwa kila anaeingia na kutoka mkoa wa Kagera.
Mwisho, ACT Wazalendo inawataka wananchi wa Mkoa wa kagera na wale wanaokwenda na kurudi mkoa huo kuchukua tahadhari na kutopuuza taarifa zinazohusu uwepo wa ugonjwa huo mpaka itakapothibitika vinginevyo.
Imetolewa na;
Dkt. Elizabeth Benedict Sanga.
Waziri kivuli wa Afya, ACT Wazalendo.
16 Januari 2025.