KITAIFA

BASHUNGWA AAGIZA KUKAMATWA KWA MKANDARASI ANAYEJENGA DARAJA LA MPIJI CHINI – DAR

BASHUNGWA AAGIZA KUKAMATWA KWA MKANDARASI ANAYEJENGA DARAJA LA MPIJI CHINI – DAR

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amemuagiza Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kinondoni (OCD), Mohamed Senkondo, kumshikilia Meneja Mradi wa Kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG), anayetekeleza ujenzi Daraja la Mpiji Chini (mita 140) pamoja na barabara unganishi (km 2.3), ahojiwe ili kuanza kuchukuliwa hatua kwa kuchelewa kuanza ujenzi wa daraja hilo na barabara unganishi.

Agizo hilo limetolewa Aprili 30, 2024 Mkoani Dar es Salaam baada ya Waziri Bashungwa kukagua athari za mvua pamoja na eneo litakapojengwa daraja la Mpiji Chini ambalo litaunganisha Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani na kutoridhishwa na sababu za kuchelewesha maandalizi ya kuanza ujenzi.

“Hatuwezi kuendelea kubembelezana, Mkandarasi huyu amekuwa mbambaishaji katika miradi yake na huu ni mradi wa tano, OCD nakukabidhi Mkandarasi huyu akatoe maelezo na awape mkataba aliousaini ili tuanze kumchukulia hatua,” amesisitiza Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Mkandarasi CRSG amekuwa mbambaishaji katika utekelezaji wa miradi mingine ya barabara ikiwemo Sanzate – Nata Mkoani Mara, barabara ya Kibaoni – Mlele Mkoani Katavi, barabara ya Amani Mahoro – Luanda Mkoani Ruvuma na pamoja na miradi mingine ambayo amepewa kazi ya ujenzi.

Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya China Railway Seventh Group kufika ofisini kwake na kueleza kuwa Serikali itaendelea kumbana Mkandarasi huyo kuhakikisha analeta mitambo na wafanyakazi wanaotakiwa katika mradi wa Daraja la Mpiji Chini ili kiangazi kitakapoanza ujenzi wa daraja hili lianze kujengwa mara moja.

Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam Eng. John Mkumbo ameeleza mkataba wa ujenzi wa daraja na barabara unganishi ulisainiwa Januari 30, 2023, na Mkandarasi kukabidhiwa eneo la ujenzi Mei 22, 2023 ambapo mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 24 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 21.

Eng. Mkumbo ameeleza kuwa vifaa vilivyoletwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi ni asilimia 46 ya vile vinavyohitajika kwa mujibu wa mkataba pamoja na wataalamu 6 kati ya 10 wanaotakiwa kimkataba ambapo kwa ujumla Mkandarasi amefanya maandalizi ya ujenzi kwa asilimia 58.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, ameeleza kuwa daraja hilo linaunganisha Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kupitia vijiji vya Maputo na Kiembeni na likikamilika litakuwa mkombozi mkubwa kwani ni muda mrefu wananchi wamekuwa wakizunguka mwendo mrefu kuingia na kutoka majumbani/kazini kwao na hata kufuata huduma za kijamii.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *