Bonanza la Pemba Lavutia Maelfu, Lengo la Kukuza Utalii wa Michezo na Utamaduni
Pemba, Zanzibar – Bonanza la Michezo na Utamaduni kisiwani Pemba limehitimishwa kwa mafanikio makubwa, likiashiria hatua nyingine muhimu katika kukuza utalii wa michezo, utamaduni, na utalii wa halal.

Katika kufunga bonanza hilo, Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvivu Zanzibar, Mheshimiwa Shaaban Ali Othman, alisisitiza umuhimu wa matamasha kama haya katika kuimarisha uchumi wa jamii na kuongeza hamasa ya utalii. “Bonanza hili ni mfano wa dhati wa juhudi zetu za kuendeleza uchumi wa buluu kupitia utalii na michezo. Limeimarisha mshikamano wa kijamii na kuleta mwonekano mpya wa Pemba kwa dunia,” alisema.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Ndugu Arif Abbas, alieleza kuwa mwaka huu bonanza hilo limepiga hatua kubwa, likishirikisha washiriki wa kimataifa kutoka Kenya katika michezo ya triathlon, duathlon, na kuogelea. Alifafanua kuwa Kamisheni ya Utalii inalenga kuifungua Pemba kupitia utalii wa michezo, utamaduni, na utalii wa halal.

“Lengo letu ni kuitangaza Pemba si tu kwa wageni wa ndani, bali pia katika soko la kimataifa. Michezo kama triathlon na gwaride la punda ni njia za kipekee za kuonyesha urithi wa Pemba,” alisema.
Matokeo ya Michezo: Triathlon: Washiriki 23. Mashindano ya kuogelea: Washiriki 56 (wanawake 18, wanaume 38). Duathlon: Washiriki 29.

Kwa ujumla, tamasha hilo limeleta mwamko mpya wa kitalii kisiwani Pemba huku likiwavutia wawekezaji na watalii wa kimataifa. Serikali na Kamisheni ya Utalii zimedhamiria kuliendeleza bonanza hilo ili liwe nembo ya utalii endelevu wa kisiwa hicho.

About Author

Bongo News

13 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *