RAISA SAID TANGA:
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Bumbuli, wilayani Lushoto limeridhia uamuzi wa kuwafukuza kazi watumishi wawili wa halmashauri hiyo na kuwapa onyo kali pamoja na kuwakata mshahara wengine watatu kwa kosa la utoro wa zaidi ya siku tano bila ruhusa ya mwajiri.
Uamuzi wa kuwafukuza na kuwapa onyo kali watumishi hao umeridhiwa na Baraza hilo katika kikao chake cha kawaida kilichofanyika bumbuli.
Maamuzi hayo yanatokana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya uchunguzi ilioundwa na Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Baraka Zikatimu kuchunguza tuhuma zilizotolewa kutoka Divisheni husika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza hili watumishi waliofukuzwa kazi ni Mhusini Khamis Mhina ambaye ni Afisa Hesabu na Nakshan Daniel Kipuyo ambaye ni Muuguzi Daraja la Pili. Wote wawili wamefukuzwa kwa kosa la utoro kazini kwa zaidi ya siku tano bila ruhusa ya mwajiri.
Watumishi watatu ambao waliopewa adhabu ya onyo ni pamoja na Patrick Peter Tarimo (Afisa Kilimo Msaidizi ambaye amepewa onyo kali la mwisho na kuwa chini ya uangalizi kwa miezi sita.
Wengine ni Reuben Gidion Singano ambaye ni Mtendaji wa KIjiji ambaye amepewa onyo kali pamoja na kuendelee na adhabu yake ya awali ya kukatwa asilimia 15 ya mshahara ghafi na kuwa chini ya uangalizi miezi sita na Stephano Augustino Syprian (Muuguzi daraja la kwanza) ambaye amepewa adhabu ya kukatwa mshahara ghafi kwa miaka mitatu.