✅️WB yaipongeza Tanzania kwa kasi ya usambazaji umeme
✅️ Tanzania yaingizwa katika mradi wa ASCENT kuongeza upatikanaji umeme
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Benki ya Dunia (WB) ukiongozwa na Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Benki hiyo, Wendy Hughes.
Mazungumzo yamefanyika jijini Dodoma ambapo viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO walihudhuria wakiongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu, Athumani Mbuttuka, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkuruugenzi wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga na wataalam mbalimbali.
Katika kikao hicho, Dkt.Biteko amewaeleza watendaji wa WB kuwa suala la upatikanaji wa umeme nchini lina umuhimu kiuchumi, kisiasa na kijamii ambapo kila mwananchi nchini anahitaji umeme, hivyo Serikali inapata msukumo mkubwa wa kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika na hivyo kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuibua na kuendeleza miradi ya nishati.
Pamoja na kuishukuru Benki hiyo kwa kutoa fedha za kuendeleza miradi mbalimbali ya Nishati ukiwemo mradi wa umeme wa Rusumo (MW 80) ambao wametoa Dola za Marekani Milioni 340 na mradi wa kuunganisha umeme kati ya Tanzania na Zambia ambao wametoa Dola za Marekani milioni 455, Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Benki kwani kumekuwa na faida zinazotokana na ushirikiano uliopo.
Dkt.Biteko ameongeza kuwa, fedha zinazotolewa na wadau wa Maendeleo ikiwemo WB zitasimamiwa ipasavyo ili zitumike kwa malengo kusudiwa na hivyo kusukuma mbele sekta ya Nishati ili kuwawezesha wananchi wote kuutumia umeme kwa shughuli za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika wa WB, Wendy Hughes, amemshukuru Dkt. Biteko kwa mazungumzo kati yao ambayo yameiwezesha Benki hiyo kueleza Dira yao ya kushirikiana na Afrika katika kuendeleza miradi mbalimbali ya nishati ikiwemo kupeleka umeme katika maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa na kueleza kuwa moja ya malengo ya WB ni kuongeza idadi ya watu wanaopata umeme.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo wa Kanda wa WB ameipongeza Tanzania kwa kuchaguliwa na kuwa miongoni mwa nchi Nne barani Afrika zilizoingizwa katika mradi wa Benki ya Dunia wa ASCENT ambao unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa wananchi.
Amesema kuwa, Tanzania imechaguliwa kutokana na kuwa na kasi kubwa ya usambazaji umeme mijini na vijijini kazi inayofanywa kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).