📌Asema Rais Samia anaendelea kuweka Historia Nchini
📌Asema Rais amenuia kupunguza changamoto za Watanzania
Na Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza Watanzania kuendeleza upendo mshikamano na kuvumiliana zikiwa nyenzo muhimu za kufikia maendeleo na ustawi wa Taifa.
Dkt. Biteko amesema hayo Kijijini kwao Bulangwa, Wilayani Bukombe Mkoani Geita alipojumuika na maelfu ya wananchi katika hafla ya kuukaribisha mwaka mpya 2025.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mambo mengi makubwa na mazuri ambayo yanahitaji kuenziwa na kuendelezwa ili kupata maendeleo ya kweli.
“Maono ya Rais Samia yamewezesha upatikanaji wa maendeleo katika sekta mbalimbali kama ujenzi wa miundombinu ya barabara, shule, vituo vya Afya na maji na hatua hii imetambuliwa kitaifa na kimataifa” amesema Dkt. Biteko
Amesemw pia kuwa maendeleo yaliyofikiwa yamepongezwa na taasisi za kimataifa zikiwemo Benki ya Dunia na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC)
Amewataka Wana Bukombe na Tanzania kuhakikisha mwaka mpya wa 2025 unaenziwa kwa kudumisha upendo, kuvumiliana na kusaidiana ili kila mmoja kuwa chanzo cha furaha kwa mwenzake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella aliishukuru serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo
Amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mhe. Dkt. Biteko kwa jitihada za kuendelea kuwa karibu na wananchi wa Bukombe na Mkoa wa Geita katika upatikanaji wa maendeleo.
” Pamoja na majukumu yako ya kitaifa, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu umeendelea kuwa nasi karibu nasi kuchochea maendeleo ya Mkoa na Jimbo letu la Bukombe” amesema Shigella
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa amepongeza kwa hatua ya kujumuika na kusherekea pamoja na wananchi na kusema hatua hiyo inawezesha wananchi kuwa karibu na viongozi wao
Naye Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila amewataka wakazi mkoa huo wasifanye makosa kitapofika kipindi cha uchaguzi.
” Tulishakubaliana kwamba mwaka huu ni wa uchaguzi Mkuu na upande wa urais tunaye Rais, Samia, Ubunge na udiwani tusifanye makosa,” amesema Kasendamila.