📌 Ashiriki ibada ya Pasaka AIC Makongoro
📌 Wakristo wakumbushwa ufufuko wa Yesu ulete mabadiliko maishani mwao
📌 Ataka wenye nia thabiti wajitokeze kugombea

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa wakristo kuliombea Taifa amani, utulivu, umoja na mshikamano uendelee ikiwa ni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 20, 2025 jijini Mwanza wakati aliposhiriki ibada ya Pasaka katika Kanisa la African Inland Church (AIC) – Makongoro.
“ Mwaka huu ni wa uchaguzi na una michakato mbalimbali ya kujiandikisha, kugombea, kupiga kura na kutangaza matokeo. Kwa niaba ya Serikali napenda kuwaomba waumini wa AICT na wale ambao tunadhani tuna uwezo wa kugombea nafasi mbalimbali tujitokeze kwa wingi tugombee, wale tu wenye nia ya kweli tuhakikishe tunawasaidia watu katika hali zao,” amesema Dkt. Biteko.
Sambamba na kugombea amewahimiza waumini kuliombea Taifa kuelekea wakati na baada ya uchaguzi “ Tujitokeze ili tuweze kugombea kwa ajili ya kuhudumia nchi yetu na wakati wa kampeni utakapofika naomba tuendelee kuliombea Taifa,”

Ameongeza kuwa Mwl. Julius Nyerere na viongozi wengine waliweka misingi imara ya amani na kushikamana wakati wote na Tanzania inafahamika duniani kote kama kisiwa cha amani hivyo waumini hao waliombee Taifa pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kufanya katika Taifa na kuendelea kufanya nchi kuwa na amani.
Amebainisha “Tuliyofundishwa kwenye ibada ya leo ni pamoja na kuwa ilikuwa kusudi la Mungu kwa Yesu afufuke na tunamshukuru Mungu kwa ajili ya siku ya leo ya kutufanya kuwa hai na sisi waumini wa Kanisa hili kukutana hapa na kuabudu kwa pamoja,”
Pamoja na hayo Dkt. Biteko amewaeleza waumini wa Kanisa hilo kuwa kufufuka kwa Yesu ni ishara ya ushindi na kuwa wote wameshinda pamoja na Yesu kama alivyoshinda mauti, watashinda pia katika kukamilisha ujenzi wa Kanisa lao ambalo wanaendelea kulijenga.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Musa Masanja Magwesela amesema waumini hao watumie nafasi ya kufufuka kwa Yesu kwa kuleta mabadiliko katika maisha yao.
Awali akihubiri katika ibada hiyo, Mchungaji wa Kanisa la African Inland Church kutoka Turkana nchini Kenya, Stephen Kilel amesema kuwa tukio la Yesu kufufuka ni tukio kuu linalowapa ujasiri wa kujua imani yao ni thabiti.
“ Wapo watu wengine ambao hawaamini kama Yesu amefufuka. Sisi tunaweza kupata matumaini makubwa kumbe maisha yetu hayaishi pale ambapo kifo cha mwili kimetupata, kuna ufufuo ambao unatupa nguvu ya kuzungumza juu ya habari njema,” amesema Mchungaji Kilel.
1 Comment
This is exactly what I was looking for—thanks for the helpful tips!