KITAIFA

DKT. MPANGO: SERIKALI ITAHAKIKISHA INAONDOA CHANGAMOTO ZA WAKULIMA

DKT. MPANGO: SERIKALI ITAHAKIKISHA INAONDOA CHANGAMOTO ZA WAKULIMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango amesema serikali itahakikisha inaondoa changamoto za wakulima
katika msimu mpya wa kilimo ikiwemo kusogeza huduma za mbolea ya ruzuku
katika maeneo ya Jirani zaidi na wakulima.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya
ya Mbinga akiwa ziarani mkoani Ruvuma. Amesema mkoa huo ni mkoa
tegemeo kwa uzalishaji wa chakula nchini hivyo ameitaka Wizara ya Kilimo
kutekeleza kikamilifu suala la upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa kiasi cha
kutosha na kwa wakati.
Amewasihi wananchi wa mkoa huo kuacha tabia ya kuuza mazao yote pasipo
kuweka akiba kwani usalama wa chakula ni vema kuanzia katika ngazi ya
kaya ili Taifa liweze kupiga hatua za kimaendeleo.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka watanzania kufanya siasa za hoja
ili kuweza kuharakisha maendeleo. Amesema utumiaji wa lugha zisizo na
staha bila kuonesha changamoto kwa hoja hupelekea uvunjifu wa amani.
Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa
utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo na kuwaasa kutunza miundmbinu
mbalimbali katika sekta za afya, elimu na maji.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amesema katika
kuimarisha kilimo cha kahawa wilayani humo , serikali inatarajia kufanya
uhakiki wa madeni ya vyama vya msingi na vyama vya ushirika ili kuwaondoa
wananchi katika adha inayowapelekea kushindwa kununua pembejeo kwa
wakati.
Mavunde ameongeza kwamba wakulima watapata mbolea ya ruzuku katika
maeneo ya jirani zaidi na kuwataka kutunza namba ya siri ili kuepusha
changamoto zilizojitokeza msimu uliopita.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango amehitimisha ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Ruvuma.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *