Naibu Katibu Mkuu (Miundombinu) wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativila akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuripoti Ofisi ya Rais-TAMISEMI. Anayeshuhudia ni Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Dkt. Charles Msonde amewataka watumishi wa ofisi yake kuwa waadilifu
katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kutekeleza azma ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa na utumishi wa
umma wenye uadilifu na tija katika maendeleo ya taifa.
Naibu Katibu Mkuu (Miundombinu) Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativila akipokea zawadi ya ua toka kwa mmoja wa watumishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bi. Angela Mgemela mara baada ya Naibu Katibu Mkuu huyo kuripoti ofisini. Wanaohududia ni viongozi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Dkt. Msonde ametoa wito huo leo kwa watumishi wa TAMISEMI mara
baada ya kumpokea Naibu Katibu Mkuu (Miundombinu) wa Ofisi ya Rais-
TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativila alieapishwa tarehe 16, Juni 2023 na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma.
Dkt. Msonda amesema, watumishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI
wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa kwani wanatekeleza
majukumu yao kwa niaba ya mwenye dhamana ambaye ni Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde akizungumza na watumishi wa ofisi yake mara baada ya kumpokea Naibu Katibu Mkuu (Miundombinu) Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativila.
“Dhamana tuliyopewa ya kuitumikia ofisi hii inatulazimu kuwa mstali wa
mbele katika kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya kiutumishi
iliyopo, hivyo tunapaswa kuhakikisha tunafanya kazi kwa uadilifu ili
tusimuangushe Mheshimiwa Rais,” Dkt. Msonde amesisitiza.
Naye, Naibu Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Charles
Mahera amemshukuru Mhe. Rais kwa kumteua Naibu Katibu Mkuu
(Miundombinu) Mhandisi Rogatus Mativila ili kuongeza nguvu ya kiutendaji
katika Ofisi ya Rais-TAMISEMI na kuongeza kuwa, ni wajibu wa
menejimenti kuhakikisha inafanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde akimkabidhi vitendea kazi Naibu Katibu Mkuu (Miundombinu) Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativila mara baada ya kuripoti Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Miundombinu) wa Ofisi ya Rais-
TAMISEMI, Mhandisi Rogatus Mativila ameiomba Menejimenti ya Ofisi ya
Rais-TAMISEMI kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake
kikamilifu.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Menejimenti ya Ofisi ya Rais-
TAMISEMI, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango, Ofisi ya Rais-
TAMISEMI Bw. John Cheyo amesema Menejimenti itatoa ushiriano wa
dhati kwa Naibu Katibu Mkuu (Miundombinu) Mhandisi Rogatus Mativila ili
aweze kutimiza wajibu wake ipasavyo.