Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Mashaka Gambo, ameonesha kujali changamoto zinazowakabili waendesha bodaboda jijini Arusha kwa kuchangia shilingi milioni 2 kwa ajili ya kulipia kodi ya ofisi ya chama chao hadi kuanzia Februari hadi Disemba 2025.

Hatua hiyo imekuja baada ya kukutana na viongozi wa waendesha bodaboda na kujadiliana changamoto wanazopitia katika shughuli zao za kila siku. Gambo amesema changamoto ya kodi ya ofisi ilihitaji ufumbuzi wa haraka ili kuepuka kero kwa waendesha bodaboda.

Mbali na mchango huo wa fedha, Gambo pia amekabidhi televisheni ya inchi 32 kwa ofisi ya chama cha bodaboda ili waendesha bodaboda waweze kufuatilia matukio mbalimbali yanayoendelea duniani. Vilevile, ametoa viti vya ofisini kwa ajili ya kuboresha mazingira yao ya kazi.

Mwakilishi wa waendesha bodaboda ametoa shukrani kwa Mbunge huyo, akieleza kuwa msaada wake ni wa kipekee na unathibitisha dhamira yake ya kuwasaidia wananchi.

“Mbunge wetu amekuwa mtekelezaji wa ahadi zake. Tunashukuru kwa TV, viti, na msaada wa kodi. Tumeahidi kushirikiana naye kwa hali na mali ili kuboresha umoja wetu,” amesema mwakilishi huyo.

Hatua ya Gambo inatarajiwa kuboresha utendaji wa chama cha waendesha bodaboda jijini Arusha na kuimarisha mahusiano baina ya serikali na wafanyabiashara hao.

About Author

Bongo News

1 Comment

    uolx90

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *