Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo, amewapongeza walimu na wananchi wa Arusha kwa kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, huku akieleza kuwa vyama vya upinzani vinavyosema kuwa hakuna miradi iliyotekelezwa vimekosa hoja ya msingi.
Akizungumza siku ya Jumatatu, Oktoba 7, 2024, katika Hoteli ya Gran Melia wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi 800 ya gesi na majiko yake kwa walimu na makundi mengine ya kijamii katika jiji la Arusha, Gambo ameweka wazi mafanikio ya Rais Samia katika sekta ya elimu jijini Arusha.
“Tunaona mafanikio makubwa katika sekta ya elimu hapa Arusha, lakini kuna wenzetu wanaosema kuwa hakuna kilichofanyika. Hii siyo kweli, kwani kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, amejenga shule mpya tano za sekondari, na nyingine ni za ghorofa. Shule ya sekondari ya Unga Limited ni ya ghorofa, na tangu uhuru eneo hilo lilikuwa halina shule ya sekondari,” amesema Gambo.
Amebainisha kuwa miradi ya ujenzi wa shule za sekondari za ghorofa pia imetekelezwa katika kata za Olmoti, Muriet (Muriet Mlimani), Sekei, na Moshono. Aidha, amejenga shule za msingi za kisasa, mfano mzuri ukiwa shule ya msingi ya ghorofa iliyojengwa Olmot.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2020, vijana walitembea kilomita 9 kuifuata shule, leo hii Rais Samia amewajengea shule mpya ya ghorofa,” ameongeza.
Gambo pia ameweka msisitizo kwa kuwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na serikali yake katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 2024.
“Tunaposema kazi iendelee, ushindi ni lazima. Tuna mambo makubwa ya kuonesha kwa wapiga kura, tofauti na wengine wanaosema tu ‘komaa kamanda’ bila kutoa ushahidi wa kazi za maendeleo,” amesema.
Hafla hiyo ya makabidhiano ya mitungi 800 ya gesi na majiko yake imefadhiliwa na Ubalozi wa China na kampuni ya Oryx Gas, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.