Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amewakabidhi Bodaboda wa Jiji la Arusha kiasi cha Shilingi 1,200,000 kwa ajili ya kutengeneza mfumo wa kuwezesha kusajili Bodaboda za Jiji la Arusha na kuwezesha upatikanaji wa taarifa za uhakika kwa ajili ya usalama na utalii.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi kiasi hicho, Gambo amesema kuwa yeye kama mbunge ni muhimu kutatua changamoto mbalimbali zinazowakumba anaowawakilisha, hivyo kukabidhi kiasi hicho ni moja ya njia za kutatua matatizo hayo.
“Mfumo huu ni kitu kizuri sana kwasababu unajua leo inaweza kutokea ajali ya bodaboda, pengine aliyepata ajali hali yake inaweza kuwa mbaya, akawa hawezi kuzungumza, unataka kumtafuta ndugu yake, taarifa unampataje? Lakini ndani ya mfumo, kuna taarifa za bodaboda na taarifa za wadhamini wake au ndugu zake”, amesema Gambo.
Nao viongozi wa Bodaboda Jiji la Arusha wakiwakilishwa na Mwenyekiti, Katibu na Mweka Hazina wamemshuru sana Gambo kwa kutatua changamoto zao kila wanapomfikishia na kuwaomba viongozi wengine waige mfano wake wa uongozi wenye kuacha alama.
“Mbunge wetu amekuwa akisaidia si tu Bodaboda, tunaona amekuwa akifanya mambo mengi kwenye vikundi mbalimbali, kwahiyo kazi anayoifanya tunaiona”, wameeleza.
1 Comment
You have brought up a very good details, thankyou for the post.