Raisa Said, Bumbuli
Shughuli za tiba katika Hospitali mpya ya Halmashauri ya wilaya ya Bumbuli, mkoani Tanga zinatarajia kuzinduliwa Septemba mosi, mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Baraka Zikatimu amaesema hapa.
Akijibu swali lililoulizwa na mmojawapo wa wajumbe wa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo wakati wa kikao cha robo ya nne, Zikatimu amesema kuwa shughuli zitakazoanza kufanyika katika Hospitali hiyo tiba kwa wagonjwa wa nje.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa Halmasharui imekwishapokea toka serikalini jumla ya Sh Bilioni1.5 kw ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
“Fedha hizo zimetolewa kwa awamu tatu ikiwa ni Sh milioni 500 kila awamu,”alisema Zikatimu na kuongeza kuwa awamu ya kwanza walipokea Sh milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Idara ya wagonjwa wa nje na maabara.
Pia wamepokea shs milioni 500 katika awamu ya pili kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma ya Mama na Mtoto na hivi sasa wamepokea fedha kama hizo kwa ajili ya ujenzi wa wodi mbili.
“Tukipata nyingine tutajenga majengo ya wadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma maalum (isolation ward),” alisema Zikatimu.
” Tunamshukuru sana Rais Samia kwa uamuzi wake wa kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya yaliyopelekea na sisi bumbuli kujenga hospital ya wilaya ambayo tunakwenda kuizindua September 1″ Alieleza zikatimu
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Amiri Shehiza, amesema kuzinduliwa kwa hospitali hiyo ni ushahidi tosha kwa wananchi juu ya sababu na umuhimu wa kuwa na Halmashauri katika eneo hilo.
Alisema uwepo wa Halmashauri unawezesha kuwepo kwa huduma kubwa na muhimu kama vile za afya kwa ukaribu zaidi. “Kuzinduliwa kwa huduma za tiba katika hospitali kutawapunguzia wananchi walioko katika kata mbalimbali za Halmashauri hiyo changamotoya ya umbali wa huduma ya Hospitali ya rufaa ya wilaya,” alisema Shehiza.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Afya, Elimu na Maji, Jumaa Dhahabu amesema kuwa kuanza kwa huduma katika hospitali hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wakazi wa Bumbuli ambao walikuwa wanategemea kwenda Lushoto au Korogwe kwa ajili ya huduma za rufaa au kwenda katika hospitali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania iliyopo Bumbuli.
“Baadhi ya huduma katika hospitali ya misheni ni ghali ambazo wananchi wa kawaida hawawezi kumudu hivyo kuanza kwa huduma za Hospitali ya Halamashauri ya wilaya ya Bumbuli kutawakomboa wananchi,” alisema,
Alisema kuwa Hospitali ya Wilaya ya Lushoto inategemewa na majimbo mawili (Lushoto na Mlalo) hivyo kuwepo kwa Hospitali ya Bumbuli kutasaidia hata wananchi wa majimbo mengine.