Inaelezwa kuwa vijana ndio wenye wajibu wa kujenga jamii na taifa. Vijana wanawajibika kuhakikisha kuwa jamii na taifa kwa ujumla linapata maendeleo kutokana na uwezo wao katika kutenda kazi, kufikiri, umaridadi katika utendaji lakini pia kutumia usomi wao kwa njia ya kisasa ambapo humfanya kijana kuwa tofauti.
Akihutubia jana jijini Dar es salaam katika kilele cha mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa ifikapo mwaka 2050 Afrika itatoa nchi 10 zenye idadi kubwa zaidi ya vijana duniani. Kwa mujibu wa World Economic Forum, zaidi ya asilimia 60 ya watu barani Afrika ni vijana walio chini ya miaka 25.
“Inakadiriwa kuwa, ifikapo mwaka 2030, Afrika itakuwa na asilimia 42 ya vijana wote duniani. Umri wa wastani kwa nchi za Afrika ni chini ya miaka 20, hii inamaanisha kuwa bara letu ni bara lenye watoto na vijana wengi. Kwa tafsiri ya kidemografia, habari hii ni nzuri na vilevile ni mbaya kwetu. Hali hii inaweza tu kuwa nzuri na yenye tija kwetu iwapo tutawekeza kwenye rasilimali watu kwa kuhakikisha uwepo wa afya bora, elimu bora yenye stadi za maisha ili kujenga nguvu kazi yenye tija kama ilivyo kwa wenzetu wa bara la Asia. Hatma yetu inaweza kuwa mbaya, iwapo hatutofanya uwekezaji sahihi” alieleza Mhe. Rais Samia.
Mhe. Rais Samia aliendelea kwa kufafanua kuwa endapo Afrika haitafanya uwekezaji sahihi itaongeza idadi ya vijana wasio na ujuzi, wasioajirika na vijana wanaokosa mwelekeo wa maisha hali itakayopelekea vijana hao kujiingiza kwenye vitendo viovu vya kihalifu na uvunjifu wa amani.
“Hali hii si ngeni kwa baadhi ya nchi zetu Afrika. Hivyo basi, kwetu sisi tuliopo hapa leo, tujiulize. Je, bara tulilorithi kwa waasisi ndilo bara tunalotaka wajukuu zetu waje kuliishi? Je, Afrika tunayoijenga leo ni yenye uchumi unaostawi au uchumi unaodumaa?, Mhe. Rais Samia alihoji.
Ni dhahiri kuwa majibu ya masuala hayo yanatatoa mwelekeo wa sera za Afrika, na hivyo Viongozi wa Bara la Afrika wanayo nafasi kubwa ya kuendelea kuijenga Afrika wanayoitaka.
“Ni wazi kuwa viongozi wenye maono hujenga sera zao kwenye maendeleo ya watu na kufuatiwa na maendeleo ya vitu. Na hapa, mniruhusu ninukuu maneno ya Baba wa Taifa hili la Tanzania. Miaka michache kabla ya kufariki kwake, Mwalimu Julius Nyerere, wakati akihutubia kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa Jijini New York alisema “Maendeleo ni watu. Watu ndio walengwa, waanzilishi na wanufaika wa chochote kinachoitwa maendeleo”. Kwa mantiki hiyo, hatuwezi kulikomboa bara letu kiuchumi, kama hatutaelekeza nguvu zetu kwenye maendeleo ya rasilimali watu, kwa kuwapa maarifa na ujuzi unaohitajika katika kuyatumia na kuyabadilisha mazingira yao kwa manufaa yao. Na huu ndiyo msingi hasa wa maendeleo na mafanikio ya bara letu”. Alibainisha Rais Samia.