Mwenyekiti wa chama cha wachangia damu kwa hiari Tanzania Dominick
Mkane akiwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) alipotembelea Taasisi hiyo jana kuangalia uhitaji wa damu uliopo.
Wadau wa afya nchini wameitaka jamii kuona umuhimu wa
kuchangia damu ili kuwezesha huduma za matibabu ikiwemo upasuaji wa
moyo kufanyika kwani changamoto ya upatikanaji wa damu imekuwa
ikipelekea wagonjwa kukosa huduma za matibabu kwa wakati.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa chama cha wachangia damu kwa
hiyari Tanzania Dominick Mkane alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kuona huduma zinazotolewa pamoja na kupata taarifa ya uhitaji
wa damu uliopo katika Taasisi hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Angela Muhozya akimuelezea namna ambavyo JKCI inapata damu kwa
ajili ya wagonjwa wake Mwenyekiti wa chama cha wachangia damu kwa hiari
Tanzania Dominick Mkane alipotembelea Taasisi hiyo jana jijini Dar es Salaam
Mkane alisema kila mtu anaweza kuumwa na kuhitaji damu wakati wowote
hivyo ni muhimu jamii ikaelewa kuwa zoezi la kuchangia damu ni la mzunguko
kwani ipo siku mchangia damu naye atahitaji damu kutoka kwa mtu mwingine.
“Sisi kama wachangia damu wa hiyari tunapenda kuungana na wataalam wa
afya wa JKCI kuifikia jamii na kuielezea umuhimu wa kuchangia damu mara
kwa mara kuwezesha matibabu ya wagonjwa wakiwemo wa moyo
wanaopatiwa matibabu hapa JKCI”, alisema Mkane.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya upasuaji wa JKCI Dkt. Angela
Muhozya alisema damu nyingi uhitajika katika upasuaji mkubwa wa moyo,
mgonjwa mmoja ili afanyiwe upasuaji anahitaji chupa tatu za damu na endapo
itatokea dharula mgonjwa anaweza kutumia hadi chupa kumi za damu
kufanikisha upasuaji huo.
Msimamizi wa wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tedy Tarimo akimuelezea Mwenyekiti wa chama cha
wachangia damu kwa hiari Tanzania Dominick Mkane uhitaji wa damu ulivyo
katika wodi hiyo alipotembelea Taasisi hiyo jana jijini Dar es Salaam
“Ili upasuaji mkubwa wa moyo ufanyike damu ya kutosha inatakiwa kuwepo
kwani katika upasuaji mkubwa wa moyo tunasimamisha moyo na kuipeleka
damu katika mashine ya kuusaidia moyo na mapafu kufanya kazi (Heart Lung
Machine)”,
“Mashine hii ni ya mipira hivyo damu inapoingia kwenye mashine inapoteza
uhalisia wake na kuna kiwango cha damu kitakuwa hakifai tena baada ya
upasuaji kufanyika ndio maana hata baada ya upasuaji mgonjwa atahitaji
kuongezewa damu tena”, alisema Dkt. Angela
Naye mgonjwa aliyelazwa katika Taasisi hiyo Mariam Selemani alisema
alimchukua mwezi mmoja kukaa wodini kusubiria damu ili aweza kufanyiwa
upasuaji mkubwa wa moyo na baada ya kufanyiwa upasuaji huo kutokana na
damu yake kuwa ndogo kidonda chake kimechelewa kupona kwa haraka.
“Damu yangu ni ya kundi “O+” na upatikanaji wake umekuwa wa shida lakini
nashukuru ilipatikana kidogo na kuniwezesha kufanyiwa upasuaji lakini hadi
sasa sijaruhusiwa kwenda nyumbani kutokana na damu yangu kuwa ndogo
nahitaji kuongezewa damu nyingine ili kidonda kipone kabisa”, alisema
Mariam.