Mbunge wa Bumbuli na Mjumbe wa Halmashauri kuu CCM Taifa January Makamba, ametoa kauli kwamba suala litakalokibeba Chama cha Mapinduzi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni namna Chama hicho kinavyoshughulika na kero zinazowakabili wananchi.
Makamba ameongeza kwamba katika uchaguzi huu kunashindanishwa mambo manne: ubora wa wagombea, ubora wa sera, ubora wa vyama, rekodi ya uongozi. Ameeleza kwamba mambo yote haya manne yanaibeba CCM. Hata hivyo, amesema kwamba uhakika wa ushindi wa CCM unatokana na namna CCM inavyoshughulikia na itakavyoendelea kuzishughulikia nakuzimaliza changamoto zinazowakabili wananchi.
Hayo aliyasema wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM katika mikutano ya hadhara ya kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa iliyofanyika katika Halmashauri ya wilaya ya a Bumbuli.
Makamba amesema wajibu wa CCM siku zote si kujihangaisha na siasa za ndani ya vyama vya wapinzani bali wajibu wetu ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa na imani na CCM kutokana na kuamini kwamba siku zote Chama na viongozi wake tutaendelea kuwasemea na kuwatetea wananchi. Bila hivyo, hata upinzani ukipasuka vipi kama Wenyeviti wetu wa Serikali za Vijiji wanawapuuza na kuwakera wananchi, ushindi wa CCM utakuwa hatarini.
“Wagombea wote tuliowateua kwa nafasi hizi za Wenyeviti ni muhimu wakazingatia dhima hiyo na dhamira hiyo na waelewe kwamba chama chao ndio kimeasisi mfumo wa utawala wa kugatua na kuleta madaraka kwa wananchi ambapo nguvu na mamlaka makubwa imepelekwa kwenye serikali za mitaa ikiwemo maamuzi yanayohusu ustawi na Maendeleo ya wananchi katika maeneo yao na hivyo viongozi wanaochaguliwa leo ni Muhimu sana katika uongozi wa nchi yetu.
Alifafanua CCM ina mfumo mzuri wa kuwapata wagombea kwani wagombea wao wanateuliwa na halmashauri kuu za wilaya ambao ni kundi la watu wengi ambao hawawezi kufanya makosa kwenye kuwapata wagombea hao
” kwenye ubora wa wagombea CCM haina shaka kabisa sababu inaleta wagombea sahii ambao imewapima na kuwachuja na wanauhakika watasimamia maslahi ya wananchi” Alieleza Makamba
Hata hivyo Makamba aliwaomba wananchi wote na wanaCCM ifikapo novemba 27 wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura na kukichagua chama cha mapinduzi ili wazidi kupata maendeleo katika maeneo yao.