KITAIFA

KAMATI YA BAJETI: YAIPONGEZA MAHAKAMA KWA KUPIGA HATUA MATUMIZI YA TEH

KAMATI YA BAJETI: YAIPONGEZA MAHAKAMA KWA KUPIGA HATUA MATUMIZI YA TEH

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa mada leo tarehe 16 Juni 2023 jijini Dodoma wakati wa mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu maboresho yanayoendelea kufanywa na Mahakama.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeipongeza Mahakama ya Tanzania kutokana na  hatua kubwa iliyopiga kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ambapo imezitaka taasisi nyingine za umma kujifunza kupitia Mhimili huo. 

Wajumbe wa Kamati hiyo wametoa pongezi hizo leo tarehe 16 Juni , 2023 jijini Dodoma wakati wa mafunzo kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania (2020/21 – 2024/25 kwa lengo la kajengea uwezo wabunge hao kuhusu maboresho yanayoendelea.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiwa katika mafunzo ya siku moja kuhusu maboresho yanayoendelea ndani ya Mahakama ya Tanzania . Mafunzo hayo yamefanyika leo tarehe 16 Juni 2023 jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo amesema Mahakama ya Tanzania inafanya vizuri katika maboresho mbalimbali ikiwemo kwenye uimarishaji wa matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya utoaji wa huduma mbalimbali, jambo ambalo   linapaswa kufanyika kwa wadau wengine wanaoshirikiana na Mhimili huo.

Kwa upande wake Mhe. Shally Raymond amesema matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli za Mahakama ziwafanya waendelee kuongeza kasi katika utoaji wa huduma na kushauri mafanikio hayo ni vema yakafanywa taasisi zingine za umma ili kuwarahisishia  wananchi kupata huduma mbalimbali.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amefafanua kwambamafanikio yaliyofikiwa katika matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli mbalimbali yametokana na utashi wa watumishi na ushirikiano uliopo miongoni mwao.

Ameongeza kuwa  mifumo mingi inayotumiwa na Mahakama imeandaliwa na wataalamu wa ndani,ikiwa na lengo la kuharakisha utoaji wa huduma ya haki kwa wananchi katika mazingira rahisi na rafiki.

Ameitaja baadhi ya mifumo hiyo ni e -Wakili ambao umesaidia wananchi kuwatambua Mawakili waliosajiliwa na kuwaepusha kutapeliwa na watu wasio Mawakili, Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri Mahakamani, mawasiliano kwa njia ya ofisi mtandao(e- office) ambayo imesaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa watumishi.

Prof. Ole Gabriel ameeleza pia baada ya Mahakama  kutumia TEHAMA ikiwemo ya Ofisi Mtandao (e-office) katika mawasiliano mbalimbali ya ndani wamefanikiwa kupunguza matumizi ya karatasi kwa asilimia 60. Hivyo  lengo ni  ifikapo mwaka 2025  matumizi hayo yafikie  asilimia 100. 

Aidha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania amewambia wajumbe wako mbioni kutumia mfumo mpya wa kutafsiri mashauri na kuandika hukumu kwa njia ya Kiswahili.

“Mfumo huu unamilikiwa na Mahakama, utatumia lugha ya Kiswahili cha Tanzania na Nchi yoyote itakayotaka kutumia itabidi ilipe Mrabaha, fedha ambazo zitakwenda kwenye mfuko Mkuu wa Serikali,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine Mtendaji Mkuu huyo  amesema kuwa wameshakamilisha ununuzi na uandaaji wa makontena 20 ambayo yatapelekwa katika Magereza mbalimbali hapa nchini. Lengo la makontena hayo ni kutaka baadhi ya mashauri yaweze kufanyika katika maeneo ya Magereza ikiwa ni mkakati wa kusaidia kumaliza na kupunguza mrundikano wa mahabusu.

About Author

Bongo News

124 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *