Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dennis Londo ameupongeza uongozi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia kwa Mtendaji Mkuu wake Mhandisi Victor Seff kwa kuwekeza miundombinu yenye tija na maslahi kwa wananchi na Taifa katika kukuza uchumi.
Mhe. Londo amesema hayo akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya ujenzi na miundombinu ya barabara inayotekelezwa katika Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mkoani Morogoro.
Amesema kuwa ujenzi wa barabara ya Ngerengere – Mkulazi- Kidunda yenye urefu wa kilometa 70.54 inayounganisha vijiji vya kata za matuli, mkulazi- na ngerengere imeondoa changamoto ya kukosa mawasiliano kwa wananchi washio katika vijiji hivyo.
“Barabara hii ni uthibitisho wa Serikali kuwaunganisha wananchi wetu kimawasilino ya shughuli za kiuchumi na kijamii zikiwemo kutoka mashambani kwenda sokoni kwa ajili ya bidhaa zao” amesema Mhe. Londo.
Amepongeza maamuzi ya TARURA ya kujenga barabara katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ili kuwakwamua wananchi kiuchumi hasa wananchi wa Mkoa wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Aidha, amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongezea Bajeti TARURA kwani kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Bajeti ya TARURA imeongezeka kwa Shilingi Bil.350.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Miundombinu) Mhandisi Rogatus Mativila ameishukuru Kamati hiyo nakuahidi kuendelea kuisimamia TARURA pamoja na kufanyia kazi maelekezo ya kamati na ushauri walioutoa kwa maslahi ya wananchi.
Kamati hiyo imehitimisha ziara yake Mkoani Morogoro ambapo miradi mbalimbali imekaguliwa ukiwemo ujenzi wa Daraja la Berega lenye urefu wa mita 140.