Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Mwenda ameahidi kuendelea kushirikiana na Walipakodi mkoani Arusha na kueleza kuwa katika mwezi Disemba ambao ni mwezi wa Shukurani kwa walipakodi hatakaa ofisini, badala yake atawafuata walipakodi kwenye maeneo yao na kuwasikiliza huku akiwapa Shukurani.

Akizungumza na mmoja wa wafanyabiasha wanaounda magari ya kubebea Watalii jijini Arusha Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyabiasha pamoja na wawekezaji katika maendeleo ya Taifa kupitia kodi wanazolipa.

Amesema kwa kutambua thamani ya walipakodi ameamua kuwafuata na kuwashukuru ili kuwapa motisha ya kuendelea kulipa kodi hali ambayo itaboresha mazingira ya walipa kodi hao wakitambua kuwa wao na TRA siyo maadui na wanajenga nyumba moja.

“Mameneja wote nimewapa maelekezo kuwa hakuna kukaa ofisini, watoke wakawasikilize walipakodi na kuona mazingira yao ya ufanyaji kazi pia kutoa Shukurani huku wakitatua changamoto walizonazo, hii itasaidia sana kuwajengea walipakodi imani” Kamishna Mkuu Mwenda.

Akiwa katika Ofisi za World Vision Tanzania mkoani Arusha Kamishna Mkuu Mwenda amesema Shirika hilo lisilokuwa la kiserikali lililoajiri wafanyakazi takribani 500 wamekuwa ni walipakodi wazuri wasiokuwa na udanganyifu katika kodi na wanaozingatia sheria.

Bw. Mwenda amesema yapo mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi za kijamii yanayofanana na World Vision lakini yamekuwa siyo walipaji wazuri wa kodi na kuwataka kuiga mfano wa World Vision kwa uaminifu katika kulipa kodi.

“World Vision inafanya kazi katika mikoa 15, angalieni uwezekano wa kwenda mikoa mingine mpaka Visiwani Zanzibar, maana mmekuwa na msaada mkubwa kwa jamii yetu hasa kwa watoto waliopo katika mazingira hatarishi na jamii zisizokuwa na uwezo” Kamishna Mkuu Mwenda.

Amewaambia World Vision kwamba milango ipo wazi kwao kufanya mazungumzo na TRA kuhusu masuala ya kikodi waliyoomba kusaidiwa na mazungumzo hayo yatafanywa kwa kufuata sheria ili kuweka usawa kwa kila upande.

Kamishna Mkuu Mwenda pia ametembelea Kampuni ya Enza Zaden Africa inayomiliki shamba za kuzalisha mbegu na kujionea uendeshaji wa shughuli zao huku akiwapongeza kwa kukua na kuwa walipakodi wa kati na waaminifu katika ulipaji kodi.

Kwa upande wao baadhi ya Walipakodi waliotembelewa na Kamishna Mkuu Mwenda wamesema ni mara ya kwanza kwao kutembelewa na Kiongozi mkubwa wa TRA na kueleza kuwa kitendo hicho kitawachagiza kulipa Kodi zaidi.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *