Baada ya miaka mingi ya usumbufu wa usafiri wa kwenda Kigamboni, serikali na kampuni ya Azam Marine zimetangaza ujio mpya wa vivuko utakaopunguza kwa kiasi kikubwa adha ya usafiri kuelekea eneo hilo.

Akizungumza katika uzinduzi wa vivuko hivyo, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema vivuko vilivyozinduliwa siku ya Jumatano tarehe 22 Januari 2025, vitaungana na vingine viwili ambavyo vinafanya kazi tayari na kufanya jumla ya vivuko vinne. Pia, amesema kufikia Mei mwaka huu, Azam Marine wataongeza vivuko vingine vinne na kufanya jumla ya vivuko kuwa vinane.

Kwa mujibu wa Ulega, kila kimoja kati ya vivuko hivyo vina uwezo wa kubeba abiria 250 kwa wakati mmoja na kutumia dakika sita kwa safari moja. Kwa wastani huo, ndani ya saa moja, kivuko kimoja kinaweza kubeba mpaka abiria 2500. Kwa vivuko vinane, maana yake abiria zaidi ya 20,000 wanaweza kusafirishwa ndani ya saa moja.

“Historia imeandikwa. Huu ndiyo ushirikiano wenye manufaa baina ya serikali na sekta binafsi. Kipekee kabisa, naomba nimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ubunifu wake na maelekezo yake kwetu kuhusu kushirikiana na sekta binafsi kuondoa kero za wananchi ndiyo zinaleta mambo kama haya,’ amesema.

Ulega amesema historia ya taabu katika maeneo yanayohitaji vivuko nchini ni ya muda mrefu, akieleza namna Watanzania walivyokuwa wakitumia kamba kuvushana kwenye maeneo hayo lakini akasema nchi sasa imepiga hatua kiasi kwamba watu wanasafiri kwa starehe kulinganisha na nchi ilikotoka.

Ulega ametumia nafasi hiyo kuipongeza kampuni ya Azam Marine kwa uwekezaji wa ‘mabilioni’ ya shilingi walioufanya katika usafirishaji wa watu kwenda na kutoka Kigamboni, akiwakaribisha pia kuwekeza katika maeneo mengine ambako uwekezaji wao unahitajika.

Azam Marine ni wawekezaji wazalendo na sisi kama serikali tunajisikia fahari kuwa nao. Ombi langu kwao na nimesikia viongozi wengine wakisema hapa ni kwamba sisi tunawakaribisha kushirikiana nao katika kuwaletea maendeleo Watanzania kwa kuondoa kero zao.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Marine, Abubakar Salim, ujio wa vivuko hivyo vipya unatarajiwa kupunguza muda wa kusubiri na kusafiri kwa abiria kutoka muda wa zaidi ya nusu saa na kuwa kati ya dakika tano mpaka sita.

Azam Marine imeonesha vivuko vyake vipya viwili ambavyo kwa kujumlisha na viwili vilivyopo, kutakuwa na jumla ya vivuko vinne vya kampuni hiyo. Akizungumza katika tukio la jana, Salim amesema matumaini ya Azam Marine ni kuhakikisha kuwa usafiri wa vivuko unakuwa ni wa uhakika na utakidhi mahitaji ya sasa na kwa miaka kadhaa ijayo.

Kwa muda mrefu, wakazi wa Kigamboni walikuwa wakitegemea usafiri wa vivuko vya serikali ambavyo sasa viko kwenye matengenezo na Azam imeleta vivuko hivyo ambavyo vinajulikana pia kwa jina la teksi za baharini kutokana na kasi yake na aina ya huduma inayotoa kwa ajili ya kuhudumia soko la abiria lililopo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametumia mkutano huo wa jana kuwataka Wanadar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kuwa na mtazamo chanya kuhusu wawekezaji kutoka sekta binafsi kwa vile wao ni washirika na kwamba wakati mwingine wanajua zaidi kuhusu biashara kuliko hata serikali.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *