KITAIFA

KIKWETE : TAALUMA YA UUGUZI  NI YA KUJITOA NA YENYE UTHUBUTU

KIKWETE : TAALUMA YA UUGUZI  NI YA KUJITOA NA YENYE UTHUBUTU

Naibu Waziri,  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa ameshika mshumaa unawakaa na baadhi ya Wauguzi  katika  shamrashamara ya kuadhimisha  Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema taaluma ya Uuguzi ni kazi ya uthubutu, utayari pamoja na kujitoa kwa ajili ya kuwahudumia  wenye mahitaji ya kiafya huku akiwataka Wauguzi kuendelea kuchapa kazi  kwa weledi na kwa kuzingatia miiko na maadili ya taaluma yao.

Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo Jumapili Julai 23, 2023 wakati akizungumza na Wauguzi wa Mkoa wa Pwani kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ambapo amewahimiza Wauguzi hao kuwahudumia wananchi kwa moyo na upendo wa hali ya juu.

Amesema, Serikali inatambua kuwa Wauguzi ni kundi muhimu sana  kwani  ndio shina na mhimili mkubwa wa utendaji na ufanisi wa sekta ya afya nchini na ulimwenguni kote.

Mhe. Kikwete ametumia fursa hiyo kumshukuru  Rais  wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi Wauguzi hao ikiwa ni pamoja na  kuweka mikakati mbalimbali ili kuyafikia malengo endelevu ya afya kwa wote.

Aidha, Mhe. Kikwete amesema Ofisi ya Rais-UTUMISHI inaendelea kuzifanyia kazi changamoto za kimuundo za taaluma hiyo na changamoto nyingine itaishirikisha Wizara husika ya Afya ili ziweze kufanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amekubali ombi la kuwa mlezi wa Wauguzi katika Mkoa wa Pwani huku akiahidi kuwapa ushirikiano ili kuwaongezea morali Watumishi hao katika kutekeleza majukumu yao.

‘’Natambua mchango wenu adhimu kwa mustakabali wa afya zetu kwani ziko mikononi mwenu, napenda kuwaahidi mimi kama mlezi wenu niko tayari kuwapa ushirikiano muda wote mtakaponihitaji” amesisitiza Mhe, Kikwete.

Awali Katibu wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Pwani, Bi, Dafroza Mnzava akisoma risala kwa Naibu Waziri Mhe. Kikwete, ameiomba Serikali kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili ikiwemo suala la muundo na posho ya mazingira hatarishi na stahiki mbalimbali.

Pia Katibu huyo ameiomba Serikali kuendelea kuajiri wauguzi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *