KITAIFA

MADAKTARI AFRIKA WATOA MSAADA WA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI MOJA

MADAKTARI AFRIKA WATOA MSAADA WA VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI MOJA

Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel akiwa katika picha ya pamoja na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani alipowatembelea kabla ya kuanza kwa kambi maalum ya siku tano ya matibabu ya umeme wa moyo leo jijini Dar es Salaam.

Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani limetoa msaada
wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni moja ambavyo vitatumika katika
kambi maalumu ya siku tano ya matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Kambi hiyo iliyoanza leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imelenga
kubadilishana uzoefu baina ya wataalam wa afya wa JKCI na wenzao kutoka
Shirika la Madaktari Afrika, kuwasaidia wagonjwa vifaa vya matibabu hayo na
kutoa huduma ya matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Akizungumza na madaktari wanaotoa matibabu katika kambi hiyo
alipowatembela leo jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin
Mollel aliwashukuru Madaktari Afrika kwa msaada walioutoa na kusemaa
magonjwa ya mfumo wa umeme wa moyo ni sehemu ngumu kwenye masuala ya
tiba ya moyo hivyo kuwapongeza madaktari hao kwa kuwa mstari wa mbele
kushirikiana na wataalam wa JKCI kuokoa maisha ya watanzania.

Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel akimsikiliza Daktari bingwa wa moyo na mfumo wa umeme wa moyo kutoka Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani David Singh alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo kwaajili ya kuonana na madaktari hao kabla ya kuanza kwa kambi maalum ya matibabu ya umeme wa moyo ya siku tano inayofanyika JKCI.


“Rais wetu alishawekeza mtambo wa kisasa wa kutibu umeme wa moyo, upande
wa suala la tiba tumejitahidi kupata wataalam wenye uwezo wa kutoa huduma
bora kuendana na teknolojia iliyopo, hatuna budi kushirikiana nanyi kwani muda
mrefu mmekuwa mkitoa matibabu haya”, alisema Dkt. Mollel.
Dkt. Mollel alisema mbali na kubadilishana uzoefu madaktari hao wamekuja
wakijua yakuwa kuna watanzania wenye matatizo ya umeme wa moyo lakini
hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu hivyo kuleta vifaa vya matibabu
kuwatibu wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu.
“Kupitia kambi hii wataalam wetu wataenda kubadilishana uzoefu na kuendeleza
teknolojia katika kutoa huduma za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo na
kuifanya Taasisi hii kutambulika katika nchi nyingi zilizotuzunguka hivyo badala ya
kuwapeleka wagonjwa wao barani Ulaya sasa wanasaini mikataba na JKCI ili
wagonjwa wao watibiwe hapa nchini kutokana na uwezo wetu kupanda hadi
kufikia asilima 97”, alisema Dkt. Mollel.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge alisema madaktari kutoka Shirika la Madaktari Afrika
wamekuja na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni moja ili kuwasaidia
wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo.
“Madaktari Afrika ni marafiki zetu ambao wamekuwa wakishirikiana nasi kwa
muda mrefu, wamefika hapa kwaajili ya kuwafundisha madaktari wetu na
kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo
kutokufanya kazi vizuri”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema katika kambi hiyo wagonjwa wenye matatizo makubwa ya
mfumo wa umeme wa moyo watapatiwa matibabu na mabingwa hao wakiwa na
lengo la kutoa huduma za matibabu pamoja na kubadilishana uzoefu na
madaktari, wauguzi na wataalam wa kuendesha mtambo wa Cathlab.
Naye Daktari bingwa wa mfumo wa umeme wa moyo kutoka Shirika la Madaktari
Afrika David Singh alisema katika kambi hiyo wanashirikiana na madaktari wa JKCI
kujifunza mbinu mpya za matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo ili kuendana
na maendeleo ya teknolojia ya matibabu.
“Tumefika katika Taasisi hii kwasababu tuna taarifa za huduma bora zinazotolewa
kwa wagonjwa wanaotibiwa hapa, hivyo tukaona ni sehemu sahihi ambayo
tunaweza kushirikiana na kuboresha huduma zaidi”, alisema Dkt. David.
Dkt. David alisema Shirika la Madaktari Afrika litaendelea kushirikiana na
wataalam wa Afya wa JKCI kwani kwa sasa Taasisi hiyo inafanya vizuri katika utoaji
wa uchunguzi na matibabu ya moyo Afrika Mashariki na kati.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *