Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa matokeo ya Usaili wa maandishi uliofanyika Machi 29 na 30 mwaka 2025 kwa watahiniwa walioomba nafasi za kazi TRA yatatangazwa Aprili 25 kupitia Tovuti ya TRA (www.tra.go.tz) baada ya kuwasilishwa na Mshauri elekezi NBAA Aprili 23, mwaka huu.

Akizungumzia mchakato huo wa ajira za TRA leo tarehe 02.04.2025 Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali watu na Utawala Bw. Moshi Jonathan Kabengwe amesema baada ya majina kutangazwa tarehe 02 hadi 04 Mwezi Mei utafanyika usaili wa Vitendo kwa Madereva na Waandishi Waendesha Ofisi.
Amesema baada ya Usaili wa Vitendo utafuata Usaili wa mahojiano kwa kada nyingine ambao utafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 07 hadi 09 Mei, 2025 ambapo watakaofanikiwa kushinda Usaili huo wataarifiwa tarehe 18.05.2025 na kuanza mafunzo Elekezi tarehe 22.05.2025 mpaka tarehe 02.06.2025 watakapoajiriwa na kuanza kazi rasmi.
Bw. Kabengwe ameeleza kuwa katika mchakato wa usaili maombi yaliyokidhi vigezo yalikuwa 112,952 yakaongezeka maombi 71 baada ya kukata Rufaa na kufikisha idadi ya maombi 113,023 yaliyohusisha waombaji 86,314 na waliofanya Usaili wa maandishi ni waombaji 78,544 sawa na asilimia 91 ya waombaji wote na waombaji 7,770 sawa na asilimia 9 hawakufika kwenye Usaili kwa sababu mbalimbali.

Ameeleza kuwa Sera ya TRA ni ajira sawa kwa wote na ajira zilizotangazwa zitazingatia sifa na vigezo vya muomba kazi bila kujali hali ya muhusika kwamba ni Mtoto wa Maskini, Mtoto wa Kiongozi au Mtoto wa Mtumishi wa Umma ndiyo maana vituo vya Usaili viliwekwa kwenye mikoa 8 na Zanzibar ili kusogeza huduma karibu.
Aidha Bw. Kabengwe ameshukuru kuwepo kwa mrejesho kutoka kwa Jamii kupitia njia mbalimbali na kueleza kuwa kama yupo mwenye Taarifa zinazoashiria kuharibu zoezi la ajira awasiliane na TRA kupitia Sikika App, namba za Simu Bure 0800 750 075 / 0800 780 078 / 0800 110 016 au Whatsapp 0744 233 333 au E-mail huduma@tra.go.tz / services@tra.go.tz au atoe Taarifa TAKUKURU