Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, amemjibu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, kutokana na kauli yake ya kumtaka kuhudhuria vikao vya mipango vya Halmashauri na ngazi ya Mkoa ili kushiriki kujadili changamoto na maendeleo ya mkoa.
Gambo, akizungumza kwa kina, amesema kwamba yeye si mfanyakazi wa serikali bali ni mwakilishi wa wananchi aliyechaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Amedokeza kwamba vikao vinavyotambulika kisheria kwa wabunge ni vile vya Bunge na kamati zake, na si jukumu la mkuu wa mkoa kutoa maelekezo juu ya ushiriki wake kwenye vikao vingine.
“Utaratibu wa kufanya kazi kwa mujibu wa katiba, sheria na kanuni uko wazi. Mtu anayeweza kutoa taarifa ya kutohudhuria vikao vyangu ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, si Mkuu wa Mkoa. Mimi kama Mbunge ni wajibu wangu kuwasemea wananchi changamoto zao, si kazi ya kunong’onezana shida za watu,” amesema Gambo.
Mbunge huyo ameongeza kuwa anahudhuria vikao vya kikatiba na wakati wa mgongano wa ratiba, anatanguliza vikao vya chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kiko juu ya serikali.
“Mimi si mtoro. Nilihudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa ya CCM kilichogongana na kikao cha Bodi ya Barabara. Chama kiko juu ya serikali, hata Mkuu wa Mkoa anatakiwa kufahamu hilo,” amesisitiza Gambo.
Kauli hiyo ilikuja baada ya Makonda, akiwa ameambatana na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kudai kuwa kutohudhuria vikao vya mipango ngazi ya Halmashauri na Mkoa ni kitendo cha uchonganishi ambacho kinakwamisha maendeleo. Makonda alitoa kauli hiyo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Mianzini-Olemringaringa inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Hata hivyo, Gambo ameendelea kusisitiza kuwa anawajibika kueleza mafanikio yaliyopatikana na kuikumbusha serikali kuhusu changamoto zinazohitaji kushughulikiwa. Aidha, amesema kuwa kauli na uelewa wa Makonda kuhusu nafasi ya Mbunge na wajibu wake zinahitaji kufafanuliwa.
“Mimi siyo mtu wa kupokea amri kwa sababu mimi ninatokana na CCM. Wajibu wangu ni kuwasemea wananchi changamoto zao kwa uwazi, siyo kunong’ona. Tunaposhirikiana na viongozi wa kitaifa ni kwa sababu hiyo ndiyo njia ya kufikisha sauti za wananchi,” ameongeza Gambo.