Zaidi ya wananchi 15 katika Kata ya Unga Limited mkoani Arusha, wamelazimika kulala nje kwa zaidi ya siku 10 baada ya moto uliotajwa kusababishwa na shoti ya umeme kuteketeza nyumba walimokuwa wakiishi.

Hali hiyo imewapa changamoto kubwa hadi pale Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo, aliposhirikiana na wadau mbalimbali kuchangia zaidi ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya kuwasaidia kupanga vyumba kwa muda wa miezi mitatu.

Mbunge Gambo, akizungumza siku ya Jumanne Novemba 26, 2024 wakati wa kukabidhi msaada huo, amesema kwamba janga kama hili linaweza kumkumba mtu yeyote, hivyo jamii inapaswa kushirikiana katika kuwasaidia waathirika wa majanga.

“Ukiangalia kwa kweli moto wenyewe ni changamoto, lakini bado pia kuendelea kubaki kwenye mazingira haya, ninadhani changamoto zinakuwa kubwa zaidi”, ameeleza Gambo,” amesema Gambo.

Ameongeza kuwa msaada zaidi wa mavazi na mahitaji mengine muhimu utatolewa na wadau kutoka Taasisi ya The Islamic Foundation, ili kuwasaidia manusura kuendelea na maisha baada ya janga hili.

Aidha, ametoa wito kwa waathirika hao kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa, hususan kuhakikisha wanapata sehemu salama ya kuishi badala ya kuzitumia kwa mahitaji mengine yasiyokuwa ya dharura.

Miongoni mwa wananchi walioathirika kwa ajali hiyo ya moto wameeleza masaibu ya yeye na wenzake wanaolala nje kwa zaidi ya siku 10, wakisema kuwa hakuna chochote cha muhimu kilichobakia zaidi ya uhai wao, hasa kwa watu ambao hawana ndugu katika eneo hilo ambao pengine wangewakimbilia kwa ajili ya kujihifadhi.

Moto huo umesababisha hasara kubwa kwa manusura, na juhudi za viongozi pamoja na wadau zimekuwa faraja kwa familia hizo huku zikihamasisha mshikamano wa kijamii katika kukabiliana na changamoto za majanga.

About Author

Bongo News

5 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *