📌Ni kufuatia hitilafu ya umeme kwenye mfumo wa Gridi
📌Aigaza TANESCO kutafuta mwarobaini wa tatizo la kufeli kwa Gridi mara kwa mara
📌Awataka kufanya ukarabati wa vituo vya kufua umeme, ili kuvipa ufanisi
📌Awatahadharisha juu ya uwepo wa mvua nyingi na kuchukua tahadhari
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amefanya ziara ya dharura katika mitambo ya kufua umeme ya Kidatu, Mkoani Morogoro kufuatia kufeli kwa mfumo wa Gridi ya Taifa jana usiku na kusababisha mikoa mingi Tanzania Bara na Zanzibar kukosa umeme.
Akiwa kwenye kituo cha Kidatu Mhe. Biteko amewataka TANESCO Kuhakikisha wanatafuta suluhisho la kufeli kwa mfumo wa Gridi ya Taifa mara kwa mara kwa kuhakikisha wanafanya upembuzi wa kina ili kuboresha miundombinu kwenye Gridi hiyo na kuongeza kuwa matatizo kama hayo yanapojitokeza yawe funzo yasijitokeze tena.
“Nawaomba radhi sana wananchi na watanzania kwa ujumla kufuatia hitilafu hiyo kwenye mfumo wa Gridi, kwani imeleta usumbufu na changamoto kwa wananchi kutokana na shughuli nyingi za kiuchumi kusimama, kutokana na kutegemea zaidi umeme, na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kwa kuchukua hatua za haraka kufika kwenye eneo la changamoto bila kusukumwa bali kwa kujiongeza.
Aidha, Mhe.Dkt Biteko, ametoa wito kwa Mkurugenzi wa TANESCO kuhakikisha timu yote ya wataalamu inashirikiana na wananchi ili kupata umeme na kuondoa changamoto hiyo na kuwapongeza kwa kufanya kazi usiku na mchana na hivyo kuhakikisha wananchi wanapata umeme na kumpongeza Mkurugenzi mtendaji wa TANESCO kwa kuchukua hatua za haraka kufika kwenye eneo la changamoto zilizojitikeza kwenye mashine za kufua umeme.
Pia, amewatahadharisha TANESCO kuchukua tahadhari hususan katika kipindi hiki cha kiwango kikubwa cha mvua zinazonyesha na kuwataka TANESCO kuchukua tahadhari kwani maji yanayoingia kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ni kikubwa na kutolea mfano wa kituo cha kuzalisha umeme cha Julius Nyerere ili kuondoa madhara yanayoweza kusababishwa na wingi wa maji hayo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Danstan Kyoba amewashukuru Wizara ya Nishati kwa hatua ilizochukua kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa wakati na kuwatahadharisha wananchi kuchukua tahadhari kufuatia kiwango kikubwa cha mvua zinazoendelea kunyesha na hivyo kuharibu miundombinu mbalimbali.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la umeme Tanzania TANESCO Mha. Gissima Nyamo-Hanga amewaomba radhi watanzaia kwa kukosekana kwa huduma ya umeme kufuatia hitilafu hiyo kwenye Gridi ya Taifa na na ustahimilivu walioonyesha katika kipindi chote cha dharura, kuongez kuwa wataalamu wa Shirika wamepambana ili kurejesha mikoa yote kwenye mfumo wa Gridi ya Taifa.
Aidha amempongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt.Doto Biteko kwa kuacha shughuli zake na kuja kuungana na wataalamu wa TANESCO kuhakikisha wananchi na watanzania wanapata umeme, na kuongeza kuwa mikoa yote imerejeshwa kwenye mfumo.
Hadi jioni hii, mashine tatu kati ya nne za kufua umeme katika Kituo cha Kidatu zilikuwa zimerejeshwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa na hivyo matarajio ni kumaliza tatatizo ndani ya muda mfupi.