Wananchi wa Kisiwa cha Pemba wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupima na kutibiwa magonjwa ya moyo katika kambi maalum ya matibabu inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani Kisiwani humo.
Rai hiyo imetolewa leo na Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tulizo Shemu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi ya matibabu ya siku tano iliyoanza leo katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee.
Kiongozi wa timu ya madaktari kutoka Jamhuri ya Serikali ya watu wa China ambao wanafanya kazi Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba Dkt. Jiang Jinhua akizungumza wakati wa kikao cha kuona jinsi ambavyo kambi maalum ya matibabu ya moyo itakavyofanyika katika Hospitali hiyo. Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Abdulla Mzee wanafanya kambi ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa Pemba.
Dkt. Shemu ambaye amemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge alisema wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee wanatoa huduma bobezi za matibabu ya moyo kwa wananchi na watahakikisha kila anayehitaji kupata huduma hizo anazipata kwa wakati.
“Tunataka wananchi wote wenye matatizo ya moyo wafikiwe na huduma bobezi, hivyo basi tumeamua kuwafuata mahali walipo kwani wengine wanashindwa kuzifuata huduma hizi Dar es Salaam kutokana na changamoto mbalimbali za maisha”.
“Tumeambatana na wataalamu mbalimbali wakiwemo wa kutibu na kufanya vipimo vya moyo, tukimgundua mgonjwa anashida tunamtibu hapahapa na kwa wale watakaokuwa na matatizo makubwa tutawapa rufaa kuja kutibiwa katika Taasisi yetu”, alisema Dkt. Shemu.
Baadhi ya wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi hiyo Dkt. Pedro Pallangyo wakati wa kikao cha kuona jinsi ambavyo kambi maalum ya matibabu ya moyo itakavyofanyika katika Hospitali ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba. Wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Abdulla Mzee wanafanya kambi ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa kisiwa hicho.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Pedro Pallangyo alisema watu wengi wanaokwenda Hospitali kupata huduma za matibabu ya moyo wanakuwa tayari wameshapata madhara ya ugonjwa huo.
Dkt. Pedro alitoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kuepuka kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo na pale watakapoona kuna kampeni ya kutoa huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali wajitokeze kupima afya zao.
“Unaweza kuepuka kupata magonjwa ya moyo kwa kuacha kutumia bidhaa aina ya tumbaku, unywaji wa pombe uliokithiri, kuepuka kuwa na uzito uliopitiliza na ili moyo wako uwe na afya njema fanya mazoezi japo nusu saa kwa siku na kula chakula bora zikiwemo mbogamboga na matunda”, alishauri Dkt. Pedro.
Kwa upande wake Msaidizi Daktari Dhamana wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee Mohammed Faki Salehe alisema wamefurahi kuwapokea wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ambao watashirikiana nao kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi.
Dkt. Salehe alisema matatizo ya moyo yapo katika ukanda wa Pwani na katika Hospitali hiyo huduma za matibabu ya moyo zipo lakini hazitoshelezi kwani wanadaktari mmoja ambaye anakliniki mara mbili kwa wiki kwa siku za Jumanne na Alhamisi na wagonjwa wanaofikiwa ni wachache.
“Kupitia kambi hii wananchi wengi watafikiwa na huduma za upimaji na matibabu ya moyo na tumewapokea watu kutoka nje ya Pemba, ninamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuhakikisha wananchi wa Kisiwa cha Pemba wanafikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo”.
“Huduma hii inatolewa bila malipo yoyote yale wananchi wanafanyiwa vipimo vya moyo na wale wanaokutwa na matatizo wanafanyiwa vipimo vya maabara, X-Ray ya kifua na CT- Scan na kupewa dawa za kwenda kutumia”, Dkt. Salehe.
Dkt. ZHU Yinjun daktari bingwa wa moyo kutoka Jamhuri ya Serikali ya watu wa China ambaye anafanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee alisema kuwepo kwa kambi hiyo kutamsaidia kubadilishana uzoefu wa kazi na wagonjwa wengi kutibiwa kwa wakati mmoja.
Nao wananchi waliofanyiwa vipimo na kupata matibabu katika kambi hiyo waliishukuru Serikali kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewapunguzia gharama za kwenda Dar es Salaam kufuata huduma ya matibabu.
“Ninashukuru kwa kupata huduma hii hapa Pemba kama ningesafiri kwenda Dar es Salaam ningetumia gharama kubwa. Nawaomba wananchi wenzangu muitumie nafasi hii kuja kupimwa na kutibiwa magonjwa ya moyo ”, alishukuru Rehema Shamte mkazi wa Chakechake.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikitoa huduma za tiba mkoba zijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kufanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo ambapo tangu kuanza kwa huduma hii mwishoni mwa mwaka jana imeshatoa huduma hiyo katika mikoa ya Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Kisiwa cha Unguja, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Manyara na Pwani.