KITAIFA

PINDA ASITISHA MPANGO WA WATUMISHI KUJIMILIKISHA ENEO LA UWEKEZAJI SAME

PINDA ASITISHA MPANGO WA WATUMISHI KUJIMILIKISHA ENEO LA UWEKEZAJI SAME

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amesitisha mara moja mpango wa Halmashauri ya Wilaya ya Same kuchukuwa eneo la wananchi wa kijiji cha makanya lenye ukubwa wa Ekari 4,000 lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda bila kushirikisha wananchi hao kwa madai kuwa ni wawekezaji.

Pinda ametoa kauli hiyo Wilayani Same mkoani Kilimanjaro leo tarehe 17 Agosti 2023 wakati alipofanya kikao na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same na kubaini mpango huo wa Watumishi wa umma kujigeuza wawekezaji katika eneo hilo kwa kujimilikisha kwa gharama zisizokuwa na tija.

Kitu cha ajabu ni kwamba watumishi wa umma mmegawana ekari 4,000 kwa kupangisha kila mmoja ekari 25 kwa malipo ya shilingi milioni moja tu kwa kipindi cha miaka 20 hadi 25, yaani kiasi hiki cha fedha kwa watumishi mnaojiita wawekezaji hakina tija yoyote kwa Taifa Amesema Naibu Waziri Pinda.

Mhe. Pinda amesitisha mpango huo wa watumishi wa Serikali kujimilikisha eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na badala yake kulifanya kuwa la kilimo bila makubaliano ya wananchi huku watumishi wa umma kujigeuza wawekezaji jambo ambalo lilipingwa na wananchi wa eneo hilo.

Nashaa sana kuona watumishi wa Serikali ndio mnataka kuwa chanzo cha mgogoro wa ardhi kwa Kitendo cha kulibadilishia mpango wa matumizi ya ardhi ya uwekezaji kuwa ya kilimo cha vitalu vya katani kitendo ambacho kilipingwa na wananchi sababu walitenga eneo jingine ambalo lingeweza kutumiwa kwa ajili ya kilimo Aliongeza Mhe. Pinda

Kilichomshangaza zaidi Mhe. Pinda ni maamuzi ya kujikodishia maeneo haya  watumishi wa Serikali peke yao bila kuwashirikisha  wananchi tena kwa gharama ya milioni moja kwa hekari 25 kwa malipo ya kipindi cha miaka 20 hadi 25, gharama ambazo ni ndogo sana na hazina maslahi yoyote kwa jamii na Taifa.

“Nimeshangaa sana kuona kumbe bado kuna watendaji wa Serikali ambao wanaanzisha migogoro ya ardhi makusudi badala ya kuzuia kwa kushindwa kuheshimu mipango ya matumizi ya ardhi iliyowekwa na mamlaka zetu za vijiji kwa vigezo vya kuwapa wawekezaji ambao ukichunguza ni watumishi wa Halmashauri wanaojimilikisha” Alisema Pinda.

Nakuagiza Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni kuhakikisha unafuatilia kwanini Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same amebariki mpango huu mbovu ambao hauna masilahi kwa wananchi na hata Halmashauri yenyewe kujinyima mapato Aliongeza Pinda.

Aidha, Naibu Waziri Pinda amemuelekeza pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Same Anastazia Tutuba kuhakikisha eneo linguine lililotengwa kwa ajili ya michezo lirudishwe kwenye matumizi yake halisi kwani Halmashauri ya Wilaya ya Same ilibadilisha matumizi ya eneo hilo na kulifanya kuwa eneo la mnada.

Katika hatua nyingine Pinda amevitaka vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuchunguza mara moja juu ya  maamuzi hayo mabovu ya kubadilisha matumizi ya ardhi katika kijiji cha Makanya kutoka uwekezaji wa viwanda  na kufanya kuwa eneo la uwekezaji wa kilimo tena kwa watumishi wenyewe kwa masilahi yasiyo ya wananchi na hata Halmashauri yenyewe 

Mh Naibu Waziri amewaasa watumishi kote nchini kuhakikisha inasimamia vyema kuondoa migogoro ya ardhi katika maaeneo yao badala ya wao kuwa vyanzo vya kuanzishwa kwa migogoro hiyo.

Ameeleza pia nia ya Serikali ya Awamu ya sita ni kujaribu kupambana na migogoro ya ardhi hapa nchini ambalo limekuwa tatizo sugu na amewataka watumishi wa Serikali kuzingatia maadili ya kazi yao.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *