📌 Asema lengo ni kuwa na uhakika wa kuendeleza Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia

📌 Afunga Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Afrika Mashariki

📌 Ataka Rasilimali na Mafuta na Gesi Asilia kuchangia maendeleo ya Sekta nyingine

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amezihamasisha nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa na Mifuko ya Maendeleo ya Petroli (Petroleum Fund) ambayo itasaidia katika utafiti, ubunifu, mafunzo na uendelezaji wa Sekta ya Mafuta kwa ujumla.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo tarehe 07 Machi 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifunga Kongamano na Maonesho ya Petroli Afrika Mashariki (EAPCE’25) ambalo limefanyika kwa Siku Tatu.

Ameeleza kuwa, Dira ya Afrika Mashariki ya 2050 inaelekeza kuhusu kuanzishwa kwa Mfuko huo wa Petroli hivyo huu ni wakati muafaka wa kutekeleza suala hilo kama lilivyoainishwa katika Ibara ya 114 ya Mkataba wa Afrika Mashariki ambayo inaelekeza kuimarisha mashirikiano katika kusimamia rasilimali kwa faida ya wote.

“Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimejifunza kutoka Umoja wa Wazalishaji wa Mafuta Afrika (APPO) kwa kushirikiana na Benki ya Afrexim ambao wamekubaliana kuanzisha Benki ya Nishati ya Afrika (AEB) ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ufadhili ya miradi ya mafuta na gesi kwa kigezo cha kuchangia katika mabadiliko ya tabia nchi.” Amesema Dkt.Mwinyi

Rais Mwinyi pia ameeleza kuhusu umuhimu wa Rasimali za Mafuta na Gesi Asilia kuwa na mchango katika ukuaji wa Sekta nyinginezo akitolea mfano jinsi Sekta ya Mafuta nchini ilivyosaidia miradi ya umeme hasa usambazaji wa umeme vijijini.

Aidha, amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kujitolea kwake bila kuchoka katika maendeleo ya sekta zote ikiwemo mafuta na gesi ambapo chini ya uongozi wake miradi ya kimkakati katika Sekta hiyo imeendelea kutekelezwa.

Pia, amezipongeza Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufanya mkutano huo kwa mafanikio ikiwemo Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamati ya kitaifa ya EAPCE 2025, Timu ya Kitaifa ya Uratibu na kamati zake ndogo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Biteko amesema Mkutano huo umehusisha majadiliano, kubadilishana mawazo, kuwasilisha mawasilisho kutoka kwa Wataalam wa Sekta ya Mafuta na Gesi na kuangazia namna bora kutumia rasilimali za mafuta kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa uhakika, nafuu na usalama wa nishati.

Amesema Kongamano la EAPCE’25 limehudhuriwa na washriki zaidi ya 1400 kutoka nchi 25 na huo ni ushuhuda wa dhamira ya dhati ya nchi wanachama wa EAC kukuza ajenda ya nishati ya uhakika kwa maendeleo endelevu ya watu.

About Author

Bongo News

5 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *