MICHEZO

RAIS DKT. SAMIA ATUNUKIWA TUZO YA HESHIMA NA TFF

RAIS DKT. SAMIA ATUNUKIWA TUZO YA HESHIMA NA TFF

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma (kulia)
akipokea Tuzo ya Heshima kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) Ndg. Wallace Karia (kushoto) ikiwa ni kutambua mchango wake katika
kuendeleza Soka nchini.Tuzo hiyo ameipokea katika Usiku wa Tuzo Juni 12, 2023 Jijini
Tanga.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Tuzo ya Heshima ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa mchango wake wa kupenda, kuthammini na kuendeleza michezo nchini.

Tuzo hiyo imetolewa kwa Rais Dkt. Samia ikiwa ni mwendelezo wake kwenye sekta ya michezo kukutana na kuwapongeza wanamichezo wanapofanya vizuri kwenye michezo tangu aingie madarakani pamoja na kuunga mkono na kutia hamasa vilabu vya Simba na Yanga kwenye mashindano ya kimataifa kwa kutunuku kila goli lililofungwa katika mashindano ya Klabu Bingwa na Shirikisho la Mpira Afrika kwa kila goli lililofungwa maarufu kama “Goli la Mama”.

Akipokea tuzo hiyo Juni 12, 2023 jijini Tanga kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgeni Rasmi katika usiku wa Tuzo za Shirikisho la Mpira nchini (TFF) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma ameahidi kuifikisha tuzo hiyo na kusema imetolewa kwa Rais wa nchi akiwa ni shabiki namba moja na mpenda michezo nchini.

Naibu Waziri Mwinjuma ameongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga vizuri kuendeleza miundombinu ya michezo nchini kwa kukarabati viwanja saba vya Mkwakwani Tanga, CCM Kirumba Mwanza, Sokoine Mbeya, Jamhuri Dodoma, Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru vya jijini Dar es salaam na Uwanja wa Amani Zanzibar pamoja na kujenga viwanja vipya viwili nchini katika mikoa ya Arusha na Dodoma kabla ya mwaka 2027 ambapo Tanzania, Kenya na Uganda zimeomba kuwa wenyeji wa Mashindano ya Afrika (AFCON).

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira nchini (TFF) Bw. Wales Karia amesema  wanautaratibu wa kuwatambua na kuwatuza watu mbalimbali waliotoa mchango wao katika kukuza na kuendeleza soka nchini kila wanapofunga msimu wa ligi zote za mpira wa miguu chini.

Hafla hiyo ya utoaji tuzo imehudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu pamoja na Viongozi mbalimbali, wachezaji na wageni waalikwa walioshamirisha hafla hiyo.

About Author

Bongo News

34 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *