• Ni zile zilizoharibiwa na mvua za sasa nchini
• Mabilioni mengine kujenga miundombinu ya kudumu
• Ulega akatisha Bunge kujionea uharibifu Morogoro
• Atua na timu ya mainjinia ujenzi uwe wa viwango
• Aagiza mainjinia wabaki saiti usiku na mchana

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

SERIKALI ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kutumia kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ukarabati wa barabara muhimu za maeneo mbalimbali nchini zilizoharibiwa na mvua.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa taarifa hiyo lakiwa mkoani Morogoro alikoenda kwa dharura baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kuharibu barabara inayounganisha wilaya ya Ifakara – Mlimba kwenda mkoa wa Njombe.

Ulega alisema pamoja na kiasi hicho cha fedha kilichoidhinishwa na Rais kwa ajili ya ujenzi wa dharura, mipango ya serikali ya ujenzi wa kudumu wa barabara na madaraja inaendelea kama ilivyo na haiathiriwi na mipango hii ya dharura.

“Nimekuja kwenu wananchi wa Morogoro – na hasa nyinyi wa Ifakara, Malinyi, Ulanga na Mlimba, kuwafikishia salamu za Rais wenu na pole zake kwa taabu hii mliyoipata. Lakini nimekuja pia na habari njema.

“Rais wenu, Samia Suluhu Hassan, amekubali matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa dharura wa barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mvua hizi zinazoendelea, hapa kwenu na maeneo mengine ya Tanzania, ili maisha yenu yaendelee. Barabara ni uchumi. Barabara ni maisha na lazima kazi ziendelee,” alisema.

Ulega aliyelazimika kukatisha kuendelea na vikao vya Bunge vinavyoendelea mkoani Dodoma kwa ajili ya kufanya safari hiyo ya dharura, alifuatana na baadhi ya wahandisi wabobezi nchini kutoka wizarani na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili wasimamie viwango kwenye ukarabati utakaofanyika.

Kabla ya kuzungumza na wananchi wa Ifakara na viongozi waliokuwepo kwenye eneo barabara ilikokatika, Ulega alifanya ziara kwa njia ya helikopta akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, kuona athari za mvua kwenye miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo.

Baadhi ya miundombinu ya Morogoro kama madaraja, itafaidika pia na mpango wa serikali wa ujenzi wa madaraja na barabara wa kudumu unaoendelea nchini baada ya miradi yake kuridhiwa na serikali ya Rais Samia.

Baadhi ya barabara za Morogoro zitakazofaidika na mpango huu wa serikali ni Ulanga – Namhanga ambayo imetengewa zaidi ya shilingi bilioni 6.3 na Malinyi mpaka Mto Fulua iliyotengewa shilingi bilioni 12.

Katika taarifa yake kwa waziri, Malima alisema mkoa wa Morogoro ni mkubwa na maombi yao kwa serikali ni kwamba barabara muhimu zijengwe katika hali ambayo zitaweza kupitika na si lazima ziwe za lami.

About Author

Bongo News

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *