Mwenyekiti wa Kamisheni ya Tume ya Maendeleo ya ushirika nchini Tanzania AbdulMajid Musa Nsekela ameeleza kuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na maelekezo yake mbalimbali yamefanikisha kutafsiriwa kwa huduma na bidhaa mbalimbali za vyama vya ushirika nchini, akisisitiza uadilifu katika kulinda na kutunza mali za Vyama vya ushirika pamoja na mtaji wa Benki ya Ushirika ili kufanikisha dhamira njema ya Rais Samia.

Wakati wa uzinduzi wa benki hiyo ya ushirika leo Aprili 28, 2025 Jijini Dodoma kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Nsekela ameeleza kuwa ni maono ya Rais Samia pia kutaka kuona ushirika unaojiendesha kibiashara kwa lengo la kumuunganisha kila mwana ushirika na zaidi kwenye sekta mbalimbali ambazo hazijaingia kwenye mfumo rasmi sambamba na kushughulikia changamoto zao.

Akielezea pia dhamira ya Rais Samia, Nsekela amesema Rais anatamani kuona ushirika wenye mawazo chanya, akisema kazi ya Kamisheni ya Ushirika inayoendelea kwasasa ni kuhakikisha wanaondoa taswira hasi iliyokuwepo na kuwafanya wakulima kuona ushirika ni biashara, utakaojiendesha kwa weledi, usimamizi unaoleta tija na uwajibikaji.

Kuhusu Vyama vya ushirika kuonekana kuwa na ubadhirifu kwenye ripoti nyingi za Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali CAG, Nsekela ameeleza kuwa kazi inaendelea ambapo vyama vya ushirika takribani 7000 vimeunganishwa kwenye mfumo wa Kidigitali uliobuniwa na tume ya ushirika na Wizara ya Kilimo ili kuwezesha taarifa kusomana na kupatikana kwa urahisi na kwa uwazi.

Akizungumzia matarajio ya Kamisheni ya Tume ya maendeleo ya ushirika ili kutimiza maono ya Rais Samia ya kuundwa kwa Benki hiyo ya ushirika, Nsekela ameeleza kuwa ni matarajio yao kuwa Benki hiyo itajiendesha kwa uwazi, utawala bora na uadilifu katika kuhakikisha kuwa mtaji wa Benki hiyo haupotei sambamba na kuendelea kujenga uwezo kwa Vyama vya ushirika.

About Author

Bongo News

1 Comment

    This is so helpful. Looking forward to your next post!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *