Na Mwandishi Wetu
WANANCHI wanaotumia barabara ya Same – Mkomazi wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa haraka wa daraja lililovunjika katika kijiji cha Mpirani, Same mapema mwezi huu kutokana na mvua.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameeleza kwamba kukatika kwa daraja hilo kulikata mawasiliano ya barabara kati ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro hadi Mkomazi kulisababisha usumbufu mkubwa kwao.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kumtuma Waziri wa Ujenzi kuja hapa kuangalia hali na kutoa maelekezo. Tunashukuru kwamba daraja linapitika na tunaweza kuendelea na kazi zetu kama kawaida,” alisema Hassan Mkayanda ambaye ni mkazi wa Same.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alitembelea eneo hilo wiki iliyopita na kuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kujenga daraja hilo usiku na mchana ili liweze kupitika tena na kuruhusu shughuli za kijamii na kiuchumi zirejee katika hali ya kawaida.
Barabara hiyo muhimu katika upande wa Kaskazini mwa Tanzania ni miongoni mwa zilizoathiriwa na mvua ambazo Waziri Ulega alizifanyika ukaguzi katika maeneo tofauti nchini katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.