Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.
Deogratius Ndejembi amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali
kupitia mradi wa SEQUIP imekamilisha mchakato wa kujenga nyumba 212
ili kupunguza changamoto ya upungufu wa nyumba za watumishi wa kada
za elimu na afya nchini.
Mhe. Ndejembi amesema hayo leo Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu
swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Shally Josepha Raymond aliyetaka
kujua jitihada zilizofanywa na Serikali katika kutatua changamoto ya
upungufu wa nyumba za watumishi wa kada za elimu na afya.
Mhe. Ndejembi amesema, Serikali inaendelea na jitihada za kukabiliana na
upungufu wa nyumba za watumishi wa kada za elimu na afya hususani
waliopo vijijini.
“Ni kweli kuna uhitaji mkubwa wa nyumba za watumishi waliopo vijijini
hususani wa kada ya elimu na afya, hadi Mei 2023 idadi ya nyumba za
walimu zilizopo vijijini ni 55,097 wakati upungufu ni nyumba 255,097 na
idadi ya nyumba za watumishi wa kada za afya zilizopo vijijini ni 7,818 na
upungufu ni 15,272,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa, ni wajibu wa halmashauri kuanza
kutenga fedha katika mapato yao ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa nyumba
za watumishi wa kada ya elimu na afya ili kuunga mkono jitihada za
Serikali kuu kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan ameshapeleka fedha vyingi kwa ajili ya ujenzi wa
maboma, madarasa, zahanati na vituo vya afya katika halmashauri zote.