Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Peter Kisenge akimuelezea Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe
maendeleo ya ujenzi wa jengo la Utawala na vipimo alipotembelea jengo hilo leo
kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi.
Shilingi bilioni 3.6 zimetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suhulu Hassan kujenga jengo la Utawala na vipimo
ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI).
Jengo hilo linalotarajiwa kumalizika mwezi Agosti mwaka huu linatarajiwa kutoa
huduma za vipimo kwa wagonjwa zaidi ya 200 kwa siku hivyo kupunguza muda
wa kusubiri huduma za vipimo na matibabu ya moyo.
Mkandarasi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Baraka Killungu
akimuelezea Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe maendeleo ya
ujenzi wa jengo la Utawala na vipimo la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
alipotembelea jengo hilo leo kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi
Akizungumza alipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuangalia
maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif
Shekalaghe alisema kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za matibabu ya
moyo Mhe. Rais alitoa fedha hizo ili kuhakikisha kuwa huduma za matibabu ya
moyo zinaboreshwa hapa nchini
“Jengo moja lililopo kwa sasa linahudumia wagonjwa wa nje, linatoa huduma za
vipimo, kutoa huduma za upasuaji wa moyo pamoja na kulaza wagonjwa hivyo
kuleta msongamano mkubwa kwa wagonjwa wanaopata huduma JKCI”, alisema
Dkt. Shekalaghe.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe akimpa maelekezo
Mhandisi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Eng. Haji Mbuta baada ya
kutembelea ujenzi wa jengo la utawala na vipimo la Taasisi hiyo leo katika Taasisi
hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam
Dkt. Shekalaghe alisema Wizara inafuatilia hela zinazotolewa na Mhe. Rais ili
ziweze kukidhi mahitaji yaliyokusudiwa kwa wakati hivyo kuwataka wakandarasi
wa ujenzi huo kufanya kazi usiku na mchana ili ujenzi uweze kukamilika kwani
Mhe. Rais anapenda anapotoa fedha zitumike kama zilivyopangwa ili aweze kutoa
tena fedha nyingine katika kuboresha sekta ya afya.
“Hadi sasa jengo hili limekamilika kwa asilimia 71, natambua kwamba ujenzi huu
upo nyuma ndani ya mwezi mmoja kwani lilitakiwa kukamilika mwezi Mei mwaka
huu, baada ya ziara ya leo naomba kusiwe na changamoto nyingene tena kuzuia
jengo hilo kukamilika mwezi Agosti”, alisema Dkt. Shekalaghe
Aidha Dkt. Shekalaghe amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI kuhakikisha kuwa
vifaa vinavyohitajika katika jengo hilo vinaandaliwa mapema ili jengo
linapokamilika mwezi wa nane lianze kutumika hapo hapo na kusiwe na
changamoto za kusubiria vitendea kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge alisema kumekuwa na uhaba mkubwa wa ofisi pamoja na
vyumba vinavyotoa huduma za vipimo vya moyo hivyo Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotembelea Taasisi
hiyo mwaka 2021 kwa ajili ya kuzindua mtambo wa Cathlab akawiwa kutoa fedha
hizo lengo likiwa kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo.
Dkt. Kisenge alisema wagonjwa wa moyo wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu
kupata huduma za vipimo vya moyo hivyo kumalizika kwa jengo hilo kutawapa
nafuu wagonjwa kutokusubiri huduma za vipimo hasa upande wa kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO).
“Mitambo itakayowekwa katika jengo la utawala na vipimo vya moyo itakuwa
mikubwa na ambayo inachukua muda mfupi kutoa huduma za vipimo na majibu
ambapo tunatarajia ndani ya masaa mawili mgonjwa anaweza kuwa
ameshafanyiwa vipimo, kupatiwa majibu yake, na kumuona daktari”, alisema Dkt.
Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema jengo la utawala na vipimo litatoa huduma za maabara,
huduma za vipimo vya ECHO na ECG, eneo maalum kwa ajili ya wagonjwa
wanaotoka nje ya nchi (Medical Tourism), lakini pia kama alivyoshauri Katibu
Mkuu Wizara ya Afya kutakuwa na vyumba vya madaktari kwa ajili ya kuwaona
wagojwa ili kuwapunguzia mzunguko wagonjwa.
Naye Mkandarasi wa jengo hilo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Baraka
Killungu alisema jengo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 1400 lina ghorofa 4
ambapo kila ghorofa lina ukubwa wa mita za mraba kati ya 290 hadi 330.