Naibu Katibu Mkuu (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa Dkt. Charles Msonde amesema taifa linawategemea walimu wa
elimu ya awali na msingi kuwajengea msingi bora wa malezi watoto ili
wawe na maadili mema yatakayowawezesha kutoa mchango katika
maendeleo ya taifa.
Dkt. Msonde amesema hayo wakati akifungunga mafunzo ya walimu wa
elimu ya awali 202, Maafisa Elimu Kata 36 na Walimu Wakuu 36 wa Mikoa
ya Shinyanga na Simiyu yaliyolenga kuwajengea uwezo watendaji hao
kutoa elimu bora kwa watoto.
Dkt. Msonde amesema, Serikali inatambua mchango wa walimu wa elimu
ya awali na msingi na ndio maana kupitia mradi wa BOOST inajenga
miundombinu ya elimu na kuandaa mafunzo yatakayowaongezea umahiri
katika kutoa elimu bora kwa watoto.
Ameongeza kuwa, Serikali imejipanga kuboresha elimu kufikia kiwango
cha juu ndani ya muda mfupi ili kuwa na taifa imara lenye rasilimaliwatu
yenye tija.
“Nimejionea zana na kuelezwa namna mlivyofundishwa kutumia na
kutengeneza zana za kufundishia watoto, na mwalimu mzuri ni yule
anayeweza kubuni zana za kufundishia kutokana na mazingira aliyopo,”
Dkt. Msonde amesisitiza.
Kwa upande wake, mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo, Mwalimu
Mary Mapembe amesema wamejifunza zana 11 za kufundishia watoto
akitoa mfano wa zana ya mti wa namba na irabu ambayo itawasaidia
kuwafundisha watoto kusoma na kuhesabu.
Naye, Mwezeshaji Mkuu, Bi. Alphoncina Pembe amesema walimu hao
wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuwajumuisha wanafunzi wenye
mahitaji maalum ndani ya madarasa ya kawaida na kuongeza kuwa,
wamefundishwa namna ya kuchopeka masuala mtambuka wakati wa
kufundisha.