Na Mwandishi Wetu, Dar
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Crispin Francis Chalamila leo tarehe 14/01/2025 amesema Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kuhakikisha Kodi ya Serikali inakusanywa kikamilifu.
Akiwa katika mazungumzo na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda alipomtembelea ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TAKUKURU amesema licha ya kushirikiana na na TRA katika kuhakikisha Kodi yote inakusanywa pia watahakikisha Kodi hiyo inatumika kwa ajili ya matumizi yaliyopangwa na Serikali.
Chalamila amesema TAKUKURU na TRA ni Taasisi muhimu kwa ustawi wa nchi hivyo ushirikiano wao utakuwa na tija katika kuisaidia Serikali kuleta maendeleo kwa Wananchi.
“Maendeleo tunayoyaona nchini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya Elimu, Afya na Miundombinu ni matokeo ya wazi ya Kodi zinazokusanywa na TRA hivyo inapaswa kuungwa mkono na kuielimisha jamii itambue kuwa hiki ni chombo chao” amesema Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mwenda ameishukuru TAKUKURU kwa ushirikiano wanaouonyesha kila panapohutajika katika kuhakikisha majukumu ya TRA hayakwami.
Amesema TRA imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na TAKUKURU katika kuhakikisha hakuna Kodi inayokwepwa huku wakiziba mianya ya rushwa na ukwepaji Kodi na kuchukua hatua stahiki kwa wanaobainika kukutwa na hatia za rushwa na ukwepaji wa Kodi.
“Tunaishukuru sana TAKUKURU kwa ushirikiano wao wa muda wote katika kuhakikisha Kodi yote inakusanywa kwaajili ya maendeleo ya Taifa na kuweka msukumo katika usimamizi wa matumizi sahihi ya Kodi hizo” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.