Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na
viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa Mawasiliano kwenye hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Mkongo wa Baharini cha Airtel 2Afrika pamoja na Mtandao wenye kasi ya 5G wa Kampuni ya Mawasiliano ya Artel Tanzania iliyofanyika Mbezi Tanki Bovu Jijini Dar es Salaam tarehe 10 Agosti, 2023.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha mifumo yote ya
TEHAMA inasomana na taasisi zinazosimamia sera hizo.
Rais Samia ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa mkongo wa mawasiliano wa
2Afrika na matumizi ya teknolojia ya 5G iliyofanyika katika ofisi za kampuni ya Airtel
zilizopo Tanki Bovu.
Aidha, Rais Samia amesema misingi imara kwenye TEHAMA na mifumo ya
mawasiliano kisera, kisheria na kitaasisi itawezesha kujenga uchumi jumuishi wa
kidijitali (Digital Inclusive Economy) na kuinua maisha ya wananchi mijini na vijijini.
Vile vile, Rais Samia amesema uzinduzi wa teknolojia ya 5G itarahisisha utoaji wa
huduma mbalimbali, ikiwemo utunzaji taarifa muhimu, ukusanyaji maduhuli ya
serikali, kutuma na kupokea fedha pamoja na biashara za mitandaoni.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema kuongezeka kwa mkongo huu kutatoa
fursa kwa mitandao ya simu na watoa huduma wengine kuchagua mkongo
wanaotaka kutumia, hivyo kuongeza ubora na kushusha gharama za intaneti.
Mkongo wa 2Afrika unaunganisha bara la Asia, Ulaya na Afrika kwa urefu wa
kilometa 45,000 na kutumiwa na zaidi ya watu bilioni 3 duniani.
Serikali imeanza mradi wa ujenzi wa minara mipya 758 kwa ajili ya kupanua wigo wa
mawasiliano (coverage) itakayowanufaisha Watanzania zaidi ya milioni 8 kote nchini
na kupunguza gharama za kuweka mkongo kwenye hifadhi za barabara.