Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kiwango cha thamani ya uwekezaji Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 7.98 kwa mwaka 2022/2023 kutoka shilingi trilioni 7.5 kwa hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2022.
Amesema hayo leo (Jumamosi, Agosti 12, 2023) wakati wa maadhimisho ya miaka mitano ya mfuko huo na uzinduzi wa huduma za wanachama kidijitali, kwenye ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.
“Thamani hii ipo katika soko la hisa ambalo ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa mitaji nchini ambapo mfuko huo ni muwekezaji mkubwa wa ndani mwenye hisa katika makampuni makubwa kama CRDB Bank Plc, NMB Bank Plc, Tanzania Breweries Limited, na Vodacom Tanzania Plc. ”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Mifuko ya Hifadhi ya jamii kufanya uwekezaji wenye tija kwa wanachama na jamii inayolingana na thamani ya fedha za wanachama “Fanyeni utafiti wa kina kubaini masoko ili uwekezaji unaofanywa usilete hasara kwa mifuko. ”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii kuendelea kulipa mafao kwa wakati ili kuleta utulivu kwa wanachama. “Wazee wastaafu wasisumbuliwe, kumbukeni kuwa sisi sote ni wastaafu watarajiwa. ”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza taasisi za Serikali kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa wakati uzinduzi wa mkongo wa mawasiliano wa 2Afrika na matumizi ya teknolojia ya 5G la kutaka taasisi zote za Serikali ziwe zinasomana ili kurahisisha na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watanzania.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof Joyce Ndalichako amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maono na dhamira ya dhati ya kuimarisha sekta ya hifadhi ya jamii “lengo la Rais Samia ni kuona inafanya kazi kwa tija, ufanisi na kutoa huduma bora. *
“Tunampongeza pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa uthubutu wa kutoa fedha kwa mfumo wa hati fungani shilingi trilioni 2.17 za kulipa deni ambalo lilimedumu kwa muda mrefu, mfumo huu umewezesha PSSSF kulipa wastaafu kwa wakati,. ”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) CPA Hosea Kashimba amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano, hadi kufikia Juni, 2023 mfuko huo umelipa kiasi cha shilingi trilioni 8.88 kwa wanufaika 262,095.
Amesema kuwa kati ya Julai, 2018 na Juni, 2023 mfuko huo umeweza kulinda na kuongeza thamani yake kwa asilimia 27.76 kutoka trilioni 5.83 hadi trilioni 8.07 Juni, 2023. “Ongezeko hili ni sawa na wastani wa asilimia 6.72 kwa kila mwaka”.