WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini watoe mafunzo yanayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira.

“Mahitaji ya soko la ajira tutayajua kwa kufanya tafiti za mara kwa mara kwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa.”

Ametoa wito huo leo (Jumanne, Machi 18, 2025) katika Maadhimisho ya miaka 30 ya Uanzishwaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Amesema katika zama hizi zenye kasi ya maendeleo ya teknolojia, ni muhimu kwa VETA kuendelea kujiimarisha kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

“Toeni mafunzo ya ufundi stadi yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia, mafunzo hayo yajumuishe ujuzi wa teknolojia za kisasa zinazochochea uzalishaji wenye tija.”

Akizungumza kuhusu umuhimu wa Elimu ya Ufundi Stadi, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinaonesha kuwa takribani asilimia 70 ya ajira zote ni ajira binafsi na kwa watu wenye elimu ya ufundi stadi hasa kwenye sekta za kilimo, ujenzi, usafirishaji, na huduma za kijamii.

“Kwa upande wa nchi yetu, takwimu za ajira zilizozalishwa kati ya mwaka 2020 na 2024 zinafikia Milioni 7 ambapo ajira binafsi katika sekta isiyo rasmi imeajiri watu milioni 6.1 sawa na asilimia 87.1 ambapo wengi wao wana elimu ya ufundi stadi, na sekta rasmi imeajiri watu 907,873 (asilimia 12.9) ambapo wengi wao ni wale wenye elimu ya juu”.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Viwanda na Biashara wahakikishe ujenzi wa vyuo 65 vya ufundi unakamilika haraka.

Waziri Mkuu amesema ukamilishwaji wa vyuo hivyo vinavyojengwa na Serikali unalenga kutimiza dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha Watanzania kiujuzi.

“Ujenzi wa vyuo hivi ukikamilika, VETA itakuwa na vyuo 145 katika ngazi ya Mikoa yote 26 na Wilaya zote nchini. Vilevile, katika vyuo 80 vilivyopo, vyuo 30 vilikamilishwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita (6). Tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu kwa kazi kubwa anayowafanyia Watanzania.”

Kadhalika Waziri Mkuu ameitaka VETA ihakikishe inatangaza fursa za mafunzo zilizopo ili vijana haswa wa vijijini waweze kuzitumia. “Inawezekana kabisa kuwa, wapo vijana katika maeneo mbalimbali nchini haswa ya vijijini ambao hawana taarifa ya fursa za mafunzo zilizopo.”

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *