Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA imevunja rekodi ya makusanyo tangu kuanzishwa kwake kwa kukusanya Sh. Trilion 3.587 kwa Mwezi Desemba sawa na asilimia 103.52 ya lengo ambalo lilikuwa ni kukusanya Sh. Trilion 3.465 ambalo ni sawa na ukuaji wa asilimia 17.59 ukilinganisha na kiasi cha Sh. Trilion 3.050 zilizokusanywa Desemba mwaka 2023.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 01/01/2025 Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema mbali na kuvuka malengo ya Mwezi Desemba katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 (Oktoba-Desemba 2024) imefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. Trilion 8.741 sawa na ufanisi wa asilimia 104.63 ya lengo la kukusanya Sh. Trilion 8.354 sawa na ukuaji wa asilimia 19.05 ukilinganisha na kiasi cha Sh. Trilion 7.342 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2023/24.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema makusanyo yaliyokusanywa katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25 yanapelekea TRA kuwa imekusanya kiasi cha Sh. Trilion 16.528 katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/25 sawa na ufanisi wa asilimia 104.76 ya lengo la kukusanya Sh. Trilion 13.917 zilizokusanywa mwaka wa fedha 2323/2324.

Vilevile TRA imeandika rekodi mpya ya kuweza kufikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi 6 mfululizo katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025.

“Wastani wa kiwango Cha makusanyo kwa mwezi umeongezeka kwa asilimia 18.80 toka Sh. Trilion 2.319 mwaka wa fedha 2023/24 mpaka wastani wa Sh. Trilion 2.755 kwa mwezi mwaka wa fedha 2024/2025” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.

Kamishna Mkuu Mwenda amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa miongozo mizuri iliyowawezesha kukusanya kodi kwa hiari na kuvuka malengo kwa ongezeko la asilimia 78.78.

Bw. Mwenda ametaja mambo mengine yaliyoongeza makusanyo kuwa ni kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya RTA na wizara/taasisi na ofisi za Serikali pamoja na kuongeza ubunifu, nidhamu na utendaji kazi mzuri.

Ametaja maeneo yaliyoongoza kwa makusanyo kuwa ni Sekta ya Fedha, Sekta ya Madini na Sekta ya Viwanda pamoja na uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Amesema makusanyo waliyofanya katika kipindi cha miezi 6 ya mwaka wa fedha 2024/25 ni kiashiria cha kuwa watatimiza malengo ya makusanyo ya mwaka wa fedha 2024/25 ambayo ni wastani wa Sh. 30.04.

Ameainisha kwamba kuanzia January 2025 wanaanza kutumia mifumo ya usimamizi wa Forodha (TANCIS) ulioboreshwa na wa usimamizi wa Kodi za ndani (IDRAS) ambayo itaongeza ufanisi kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa Walipakodi kukutana na watumishi wa TRA.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema wanaposherehekea mwaka mpya anaendelea kuwashukuru Walipakodi wote na kueleza kuwa TRA ipo kwa lengo la kuwasaidia kukuza na kuboresha biashara zao ili zistawi vizuri na kuendelea kulipa Kodi.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *