Waziri wa Ujenzi nchini Tanzania Abdallah Ulega ametoa maagizo kwa wataalamu mbalimbali wa ujenzi wa Wakala wa barabara nchini (Tanroads) kuhakikisha wanafanya kazi usiku kucha ili huduma za usafiri zirejee haraka katika eneo la Somanga- Mtama.

Katika hatua nyingine, serikali pia imeahidi kusaidia abiria ambao wamekwama njiani katika barabara hiyo baada ya mvua kubwa za hivi karibuni kuharibu barabara hiyo.

Ulega amebainisha hayo leo Jumatatu alipofika kwenye eneo hilo mara baada ya jana Tanroads kutangaza kufunga kwa muda kwa barabara ya Somanga-Mtama baada ya mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha Wilayani Kilwa na hivyo kuharibu daraja la muda lililokuwa limejengwa eneo hilo.

Waziri Ulega katika maelezo yake mbali ya kutoa salamu za pole za Rais Samia Hassan kutokana na mkwamo walioupata wasafiri mbalimbali waliokwama eneo hilo, amewahakikishia kuwa serikali itatoa ulinzi na usalama kwa kipindi chote watakachokuwa hapo sambamba na upatikanaji wa huduma zote muhimu kwa binadamu.

“Serikali baada ya mwaka jana kupatikana kwa tatizo la namna hii kuanzia muda huo ilifanya kazi muhimu ya kutafuta suluhu ya kudumu na suluhu ya kudumu ni kujenga madaraja na kwa barabara hii tu tuna madaraja zaidi ya matano. Kwa Lindi peke yake Mhe. Rais aliidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni 130 kwaajili ya kujenga madaraja yaliyokatika.”

“Hili daraja ambalo limekatika hapa ni la muda tu, daraja lake kamili kwasasa lipo asilimia 48 za ujenzi wake na nguzo takribani 27 kati ya 48 zenye urefu wa mita zaidi ya 12 zimeshasimikwa ardhini.” Amesema Waziri Ulega.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amebaini uzembe katika kushughulikia dharura kwa baadhi ya watendaji wa Wizara yake, akiahidi kuchukua hatua usiku wa leo Aprili 07, 2025 ili kuwa fundisho kwa watumishi wengine wanaopewa majukumu ya kushughulikia dharura mbalimbali, akiahidi pia kutoondoka eneo hilo mpaka pale barabara itakapopitika.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *