Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mafuta ya kula yaliyotokana na alizeti wakati alipotembelea banda la wilaya ya Chunya katika maonesho ya Wakulima ya Kimataifa Nanenane kwenye uwanja wa John Mwakangale jijiii Mbeya, Agosti 3, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo iweke katika lugha rahisi andiko juu ya upatikanaji wa mitaji na pembejeo kwa wakulima na wafugaji.
“Niendelee kuzitaka Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ziandae utaratibu wa kuziweka kwenye mifumo rahisi na kuzifikisha kwa wakulima na wavuvi maelezo juu ya upatikanaji wa mitaji, kupata pembejeo kwa urahisi na kuifikia teknolojia mpya.”
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Agosti 3, 2023) baada ya kukagua mabanda ya Maonesho ya Nane Nane Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Akizungumza na wadau na washiriki wa maonesho hayo, Waziri Mkuu amesema akiwa ziarani Urusi, wiki iliyopita alikutana na mwekezaji wa mbolea ambaye anataka kuja kuwekeza nchini. “Bado mahitaji ya mbolea ni makubwa, bado tuna mahitaji ya masoko na teknolojia kwa wavuvi na wakulima. Elimu iendelee kusambazwa juu ya upatikanaji wa mbolea,” amesisitiza.
Akielezea kuhusu maonesho hayo, Waziri Mkuu amesema maonesho ya mwaka huu ni mazuri zaidi ya mwaka jana kwani ameona kuna teknolojia nyingi mpya ambazo zimebuniwa na vijana.
“Kama tutaendelea kulima na kufuga hivi, tunaweza kusema sasa sekta ya kilimo imeanza kwenda kwenye mwelekeo mzuri. Tanzania iko vizuri kijiografia na imekaa kimkakati, kwa hiyo tukiwa na uzalishaji mzuri wa chakula na mazao ya kibiashara, tukafuga kibiashara na kuvua kibiashara tutaweza kulisha nchi jirani na wakulima wenyewe wataweza kunufaika.”
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliongeza bajeti za wizara hizi mbili na ya kilimo kwa mfano imefikia bilioni 900. Niwasihi Watanzania wenzangu, tuingie kwenye biashara ya ufugaji. Leo tumeona namna ya kufuga na kunenepesha mifugo. Hili ndilo eneo tunatakiwa tulikimbilie kwani litaleta manufaa ya mtu mmoja mmoja.”
Amewataka wakazi wa Mbeya na mikoa ya jirani watumie maonesho hayo yanayoendelea kufanyika hadi Agosti 8, mwaka huu, ili kujifunza teknolojia mbalimbali mpya.
Kuhusu maelekezo aliyoyatoa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan juu ya mpango wa kuwawezesha vijana kulima kibiashara (BBT), Waziri Mkuu amesema yafanyiwe kazi na hasa suala la kufanya kazi kwenye eneo kijana alitakalo.
“Vijana waliojiunga na mpango wa BBT, walioanza mafuzo mwaka huu, wamekaribia kuhitimu. Eneo la BBT liko pia kwenye mifugo. Unaweza kupewa eneo, ukaweka mifugo na kuwanenepesha. Kubwa zaidi ni upatikanaji wa mitaji,” amesema.
Kuhusu mabenki kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi, Waziri Mkuu aliwataka waangalie uwezekano wa kushusha riba zaidi. “Nimepitia mabanda ya mabenki na kuwauliza kuhusu riba. Wengi wao wameshusha kutoka asilimia 12 au 13 ya awali na wamefika asilimia tisa. Naamini wataendelea kushusha zaidi,” amesema Waziri Mkuu ambaye alikagua mabanda ya benki za Azania, CRDB, STANBIC, NBC na TADB.
Kuhusu ushirika, Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe asimamie usajili, mapato, matumizi na mwenendo wa AMCOS ili ziweze kuleta tija kwa wakulima.
“Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri upo hapa, hakikisha AMCOS ambazo hazijasajiliwa zijulikane, na kama kweli wanataka kuanzisha AMCOS warasimishwe, lakini kama zipo ambazo hazieleweki waandalieni utaratibu ili waweze kujiunga na AMCOS ambazo zipo rasmi.”
Waziri Mkuu amesema kuwa ushirika ni mfumo mzuri ambao unaweza kuwafikia wananchi kwa namna mbalimbali ikiwemo elimu, masoko au kuwapelekea pembejeo. “Ushirika unatusaidia pia kupata sauti ya wakulima kuja serikalini ili ziweze kufanyiwa kazi, ndiyo maana tunataka ushirika huu usajiliwe”
Mapema, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema wana banda kubwa kwenye maonesho hayo ambalo wanatumia vijana kuonesha teknolojia ya kunenepesha mifugo ili kusaidia kubadilisha mtazamo wa wafugaji nchini.
“Wizara yetu tumedhamiria kuwatumia vijana, kwa hiyo tutaingia mkataba wa makubaliano na Jeshi la Kujenga Taifa ili asilimia 40 ya vijana watoke jeshini, asilimia 30 iwe ni wataalamu wetu na asilimia 30 iliyobakia iwe ni vijana kutoka maeneo mengine ya asili,” alisema.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa maonesho hayo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema hai ya uzalishaji chakula hapa nchini nzuri kwani mikoa ya uzalishaji imeongezeka kutoka mitano ya awali hadi 13.
“Sasa hivi hatuzungumzii Big 5 au Big 6 bali tuna mikoa 13 ya uzalishaji wa chakula nchini. Mikoa hiyo, mwaka huu imezalisha zaidi ya asilimia 70 ya chakula chote nchini,” alisema.