Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema ni jukumu la Watendaji wa Serikali
za Vijiji kuwatambua wananchi ambao wanastahili kuingizwa kwenye
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia mikutano ya vijiji ili kuwepo na
uwazi pamoja na kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wana
vigezo vya kuingizwa.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na
walengwa wa TASAF wa Kata ya Masaki, Kijiji cha Kisanga Halmashauri
ya Wilaya ya Kisarawe wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua
utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitazama shamba la kilimo cha mikorosho na miembe ambalo ni mradi wa walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Kisanga wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Mhe. Kikwete amesema kuwa, kuna baadhi ya wananchi ambao
wanastahili kuingizwa kwenye mradi wa TASAF wenye sifa na vigezo lakini
kutokana na kutoitishwa mikutano ya kijiji hupelekea baadhi yao kukosa
nafasi ya kuingizwa kwenye mradi huo, hivyo amewataka viongozi hao
kuendesha mikutano ya mara kwa mara ili kuondoa malalamiko ambayo
yanaweza kutokea.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akimkabidhi fedha mlengwa wa TASAF, Bi. Zubeda Omari ili aweze kukamilisha ujenzi wa nyumba yake aliyoijenga kupitia ruzuku ya TASAF
Aidha, Mhe. Kikwete amesisitiza wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali
ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa akijitahidi
kuboresha maisha ya wananchi wake kwa maendeleo ya Taifa la
Tanzania.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete anaendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa
wa Pwani kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma,
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao pamoja na kukagua
utekelezaji wa Miradi ya TASAF.