KITAIFA

WAGONJWA 10 WAZIBULIWA MISHIPA YA DAMU ILIYOZIBA, KUSABABISHA MOYO KUSHINDWA KUFANYA KAZI

WAGONJWA 10 WAZIBULIWA MISHIPA YA DAMU ILIYOZIBA, KUSABABISHA MOYO KUSHINDWA KUFANYA KAZI

Wagonjwa 10 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa
kuzibua mishipa ya damu iliyoziba katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo
ya siku saba.
Kambi hiyo iliyomalizika leo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
iliyopo jijini Dar es Salaam imefanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa
moyo na mishipa ya damu wa JKCI kwa kushirikiana na mwenzao kutoka
Hospitali ya Max iliyopo nchini India.
Akizungumzia kambi hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo
ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo imefanyika
kwa mara ya nne kwa kushirikiana na wataalam kutoka Hospitali ya Max
kuwafanyia upasuaji wagonjwa waliohitaji utaalam zaidi kutokana na mioyo
yao kuwa na uwezo mdogo wa kufanya kazi.


Dkt. Angela alisema kambi hiyo ililenga kufanya upasuaji mkubwa wa moyo
kwa watu wazima ambao wanamishipa ya moyo iliyoziba lakini pia viwango vya
ufanyaji kazi wa mioyo yao kuwa chini ya asilimia 30.
“Upasuaji ambao tumewafanyia wagonjwa hawa ni mgumu kidogo, tumekuwa
tukiwafanyia uchunguzi wagonjwa hawa na kuwakaribisha wenzetu kutoka
Hospitali ya Max ili kwapamoja tuweze kuwahudumia wagonjwa hawa lakini
pia tuweze kuongeza ujuzi wetu katika kuwahudumia wagonjwa wa aina hii”,
“Katika kambi hii wagonjwa wamepandikizwa mishipa ya moyo mitatu na
wengine zaidi ya mitatu bila ya kuusimamisha moyo kwa mafanikio makubwa
hii kwetu sisi ni hatua kubwa katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo”,
alisema Dkt. Angela
Aidha Dkt. Angela alisema JKCI inategemea kufanya upasuaji wa mshipa
mkubwa wa moyo ambao umetanuka, kubadilisha mishipa ya moyo pamoja na
kuweka mlango mpya kwa wagonjwa ambao wana matatizo ya mishipa
mikubwa ya moyo kutanuka.

Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu
kutoka Hospitali ya Max iliyopo nchini India Subhash Sinha alisema ushirikiano
wake na wataalam wa JKCI unaonyesha mafanikio makubwa tangu walipoanza
kushirikiana hadi sasa.
Dkt. Sinha alisema kupitia upasuaji wa moyo ambao amekuwa akifanya na
wataalam wa JKCI amekuwa pia akitoa mafunzo na mbinu mbalimbali za
kufanya upasuaji mkubwa wa mishipa ya moyo kwa wagonjwa ambao mapigo
yao ya moyo yapo chini ya asilimia 30 bila ya kuusimamisha moyo.
“Ujio wangu hapa JKCI kwa kawaidia huwa ni wa wiki moja, naamini hizi wiki
moja moja ninazokuja kuwasaidia wagonjwa kupata matibabu wataalam wa
JKCI nao hupata nafasi ya kujifunza kwani sasa naona mabadiliko makubwa
wakati tunafanya upasuaji”, alisema Dkt. Sinha.
Dkt. Sinha alisema anatamani siku moja JKCI iwe Taasisi kubwa Afrika
inayotegemewa na wagonjwa wa moyo waliopo Afrika kwani gharama za
matibabu ni zakawaida tofauti na zile zinazotolewa nje ya Afrika lakini pia
uwekezaji wa vifaa tiba vilivyopo katika Taasisi hiyo vinajitosheleza kutoa
huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *