BIASHARA KITAIFA

WAKULIMA WA UFUTA MKOANI SONGWE WAANZA KUONA NEEMA

WAKULIMA WA UFUTA MKOANI SONGWE WAANZA KUONA NEEMA

Songwe.

Wakulima wa zao la ufuta mkoa wa Songwe wameanza kuona tija ya kuzalisha zao hilo baada ya kuuza Sh 3678 kwa kilo moja tofauti na misimu ya huko nyuma walikuwa wakiuza sh 2000.

Wananchi hao wameanza kuona kuonja manufaa hayo baada ya kuanza kuuza bidhaa hiyo kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na kuachana na utamaduni wa kuuza kiholela kupitia madalali waliokuwa wanawanyonya.

Wakulima hao walieleza manufaa hayo,baada ya ufunguzi wa mnada wa nne wa zao hilo uliofanyika kwenye soko Kuu la ghala la Magamba waliokubaliana kuuza Kwa bei hiyo ikiwa ni rekodi ya bei kubwa kutokea ikilinganishwa na misimu mingine.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mnada huo uliosimamiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) kupitia Wizara ya Kilimo, Edwin Nyondo alisema kupanda kwa bei hiyo ni wazi serikali imedhamiria kuwainua kiuchumi Wananchi wake.

“Hapo nyuma tulikuwa tukiuza mazao yetu bila mpangilio na tulikuwa tukinyonywa kwakuwa tulikuwa tunawategemea madalali waliokuwa wajanja kushikilia bei za soko hili,”alisema

Naye Jonesia Mwapamba alisema kutokana na ufanisi wa malipo yake, anaamini itakuwa chachu katika kujiletea maendeleo ikiwemo kuongeza uwekezaji katika kilimo hicho.

“Kikubwa tunaomba viongozi wa Ushirika waendelee kusimamia uuzwaji wa bidhaa hiyo,kwa kuhakikisha makampuni yazidi kujitokeza mengi ili wakulima wapate fursa ya kuchagua bei wanazotaka,” alisema

Aliwaomba wakulima wengine kuzinduka sasa kama hawakutambua kuuza bidhaa kwa mfumo huo kunalipa huku akiwaomba viongozi wanaosimamia minada kuongeza uwazi kwenye utangazaji bei.

Wakati wakieleza hayo, Seleman Daud mnunuzi kutoka Kampuni ya TGC,alisema licha kununua bidhaa hiyo kwa bei nzuri lakini aliwataka kutunza mazao yao katika ubora.

“Yawe masafi na wasiweke na vumbi na mawe kadri tutakavyokuwa tunanunua na kuona ubora wa mazao yao tutakuwa tunapanda bei,”alisema

Alisema mfumo wa stakabadhi ghalani hata wao unawasaidia kupata mzigo mkubwa wa pamoja bila kutumia gharama kubwa kuzunguka vijijini kukusanya.

“Lakini pia unasaidia kuzuia hasara kama zamani tulikuwa tunapata hasara kwakuwa tulikuwa tunawategemea madalali kuwapa fedha kututafutia mizigo na walikuwa wanakusanya kiasi kidogo,” alisema

Kwa upande wake,Mrajisi Msaidizi wa mkoa wa Songwe,Benjamin Mwangwala alisema mnada huo ulikuwa na ushindani ambapo makampuni 17 yalijitokeza kununua zao hilo.

“Katika ya makampuni hayo matano yaaliyokuja na bei ya juu yamechukua mzigo wa tani 1555 uliokuwa sokoni, “alisema

Alisema walichokifanya walichukua makampuni matano yaliyoongoza kwa bei kujumlisha na kugawa kutafuta bei ya wastani na tukafanikiwa kupata Sh 3678 wanayoenda kulipwa mkulima kwa kilo moja.

Aidha alisema kutumia mfumo huo kunaisaidia kupata takwimu halisi za uzalishaji katika mkoa huo kwakuwa Vyama vya Ushirika vinakuwa na kumbukumbu zinazoiwezesha Halmashauri husika kujipanga.

“Faida nyingine mfumo unaimarisha ushindani wa bei kwa sababu wanunuzi wanakuwa wengi na ubora unakuwa mzuri na Halmashauri zinapata ushuru wa uhakika,” alisema

Naye,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe,CPA Cecilia Kavishe aliwapongeza wakulima hao kwa kuhamasika kutumia mfumo huo huku akieleza jitihada hizo zinatokea baada ya serikali kuendelea kutoa elimu.

“Ndio maana mnaona kila mnada watu wanaongezeka, na bei inapanda, ukiangalia mnada wa kwanza tuliuza tani 100 za ufuta wapili tani 500 lakini leo tunaongelea tani 1555 tunaona tunatoka tulikokuwepo na kufikia lengo la Halmashauri kutumia stakabadhi ghalani,” alisema

Alisema kwa hamasa hiyo wanaamini mnada unaokuja wakulima wataleta mazao yao zaidi huku akieleza mfumo huo unaiwezesha Halmashauri kupata ushuru wake moja kwa moja bila usumbufu.

About Author

Bongo News

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *