KITAIFA

​WAKUU WA WILAYA LINDI MTWARA WAZITAKA TAASISI KULIPA MADENI WANAYODAIWA NA TEMESA

​WAKUU WA WILAYA LINDI MTWARA WAZITAKA TAASISI KULIPA MADENI WANAYODAIWA NA TEMESA

Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga wa pili kulia akipewa
maelekezo kuhusu vitendea kazi na fundi kutoka Wakala wa Ufundi na
Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa Lindi mara baada ya kumaliza
kuzungumza na wadau wanaotumia huduma za Wakala Mkoani humo
katika kikao kilichofanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa.

Wakuu wa Wilaya za Lindi na Mtwara wameziagiza Taasisi zilizoko Mikoani
humo kuhakikisha wanalipia gharama za huduma wanazopatiwa na Wakala wa
Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ili kuuwezesha Wakala huo kuendelea
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Wakuu hao wa Wilaya, wameyasema
hayo kwa nyakati tofauti wakati wa vikao vya wadau vilivyoandaliwa na
TEMESA na kufanyika katika Wilaya zao kwa lengo la kuendelea
kupeana mrejesho baina ya TEMESA na wadau wake kwa ujumla ambao ni
wauzaji wa vipuri, watengenezaji wa vilainishi, Taasisi za Umma na Serikali
pamoja na watu binafsi ikiwa ni muendelezo wa jitihada za Wakala huo katika
kuboresha utendaji kazi wake ili kuhakikisha wateja hao na Serikali
wanawezeshwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi bila vikwazo vyovyote.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Hanafi Msabaha akimkabidhi tuzo mmoja wa
wadau wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa
Lindi kwa kutambua mchango wake pamoja na kulipia huduma za Wakala
kwa wakati mara baada ya kuzungumza na wadau wanaotumia huduma za
Wakala Mkoani humo katika kikao kilichofanyika katika hoteli ya Luwa
Evegreen mjini Mtwara.


Akizungumza wakati wa Kikao cha wadau Mkoani Lindi, kilichofanyika katika
katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Tarehe 22 Juni, 2023, Mkuu wa Wilaya ya
Lindi Shaibu Ndemanga amewaomba wadau hao kuendelea kupata huduma
TEMESA huku akiwataka kuhakikisha wanalipia gharama za huduma baada ya
kumaliza kutengenezewa magari yao na mitambo
”Lakini tukipata huduma tulipe, Mheshimiwa Rais hawezi kuhudumia tu kila
siku, hapana, itafika mahala Taasisi lazima ijiendeshe angalau kwa asilimia
fulani, sasa hawawezi kuwa wanaenda kuchukua vipuri huko wakufungie halafu
hulipi, wanakuja kukurekebishia wewe hulipi,wataishi vipi, na hawa tumewapa
uwezo wa kufanya shughuli zao kutegemea na malipo ambayo wanayapata,
kwahiyo tukalipe.” amesisitiza Ndemanga na kuwataka TEMESA kuhakikisha
wanakagua madeni hayo vizuri ili kuona namna yanavyoweza kulipika,
amewaomba pia kutokataa kutengeneza magari ya Taasisi ambazo zinadaiwa.
Mkuu huyo wa Wilaya pia ameipongeza TEMESA kwa maboresho ambayo
inaendelea kuyafanya katika karakana zake na kuziomba Taasisi za Umma na
wadau kuiamini TEMESA kwakuwa imebadilika na inafanya kazi kwa ufanisi

mkubwa. ”TEMESA sasa imeboreka, kwa wale ambao tumepata nafasi ya
kukagua na kusikiliza kule nje, sio TEMESA ile ambayo tulikuwa nayo miaka
iliyopita, kwahiyo niwaombe tuondoe hofu, twendeni tupeleke magari yetu
TEMESA, twendeni tuwaite maofisini kwetu warekebishe wakague viyoyozi,
waje kwenye nyumba zetu waangalie pia umeme, wana vifaa vya kisasa vya
kukagua na kutengeneza viyoyozi vyetu, wana vifaa vya kisasa vya kupima
umeme kwenye nyumba zetu, twendeni tuwatumie TEMESA.” Amesema
Ndemanga na kuongeza kuwa Wakala huo kwa sasa umebadilika na gharama
zake sasa zinaendana na soko tofauti na zamani huku akiwahakikishia wadau
wa Mkoa wa Lindi ubora wa huduma kutoka Wakala huo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Hanafi Msabaha, akizungumza na wadau
hao  Mkoani humo mwishoni mwa wiki, amewataka wadau hao  kutokata
tamaa na TEMESA, kurejesha imani yao kwa TEMESA na kuendelea kufanya kazi
nao na kama itajitokeza changamoto basi wadau hao wasisite kuileta mbele
yake ili izungumzwe na kutatuliwa. Msabaha amesema vikao vya aina hiyo viwe
endelevu kwa TEMESA kuendelea kukaa na wadau wake na kutathmini namna
wadau hao wanavozitafsiri huduma za Wakala, wapi wanakosea na wapi
wapaboreshe zaidi ili TEMESA iendelee kutoa huduma bora. Msabaha pia
amesisitiza suala la wadau hao hasa Taasisi za Umma kulipa madeni yao kwa
wakati.
”Lakini ndugu wadau, tunapopata huduma za TEMESA basi mimi niwaombe na
sisi tuwe waaminifu tulipe mapema, na mara nyingi Taasisi za Serikali na
Wakala za Serikali zinazotoa huduma zinakwama kwasababu hiyo, Taasisi ni za
kwetu wenyewe lakini tunakopa hatulipi, lakini mjue kwamba kuwa na madeni
mengi pia inasababisha Taasisi kushindwa kujiendesha.” Alimaliza Msabaha.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Lazaro N. Kilahala, akizungumza kwa
nyakati tofauti katika vikao hivyo, amesema TEMESA imekuwa ikifanya vikao
na wadau kwa ajili ya kuendelea kupeana mrejesho ikiwa ni muendelezo wa
jitihada za kuboresha utendaji kazi wa Wakala huo ili kuwezesha wateja na
Serikali kwa ujumla kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila
vikwazo vyovyote. Kilahala amesema vikao hivyo ni muendelezo kwani

TEMESA iko katika kufanya mabadiliko makubwa na lazima iwashirikishe wadau
wake katika kujua maeneo gani izidi kuyaboresha lakini pia kupeana mrejesho
kwa maeneo ambayo tayari Wakala huo umekwishaanza kuyafanyia kazi.
Kilahala ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Rasi Dkt. Samia Suluhu Hassan na
Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujumla kwa uwekezaji mkubwa ambao
inaendeleea kuufanya TEMESA, amesema kuwa Serikali imekuwa ikiendelea
kununua vitendea kazi kila mara na vimekuwa vikisambazwa kila Mkoa kwa ajili
ya kuboresha utendaji kazi wa Wakala huo. ”Karakana zetu zinaendelea
kufanyiwa ukarabati mkubwa na watumishi wetu wanaendelea kupatiwa
mafunzo, hii yote ni katika kuboresha huduma na utendaji wa Wakala, hatuna
sababu ya kurudi nyuma, uwekezaji huu unaofanyika na dhamira ya dhati ya
Serikali yetu ni kuona kwamba TEMESA inakuwa bora zaidi na inakuwa
inachangia pakubwa zaidi katika maendeleo ya nchi yetu, kwahiyo hatuwezi
kurudi nyuma.” Amesema Kilahala na kuongeza kuwa anawakaribisha wateja
katika TEMESA mpya, ambayo inafanya kazi kisasa, kwa vifaa vya kisasa,
vitendea kazi vya kisasa, TEMESA  ambayo inataka kubadilika na kuishi
matarajio ya wateja wake, sio TEMESA kwa mujibu wa Sheria bali TEMESA
inayotaka kumridhisha mteja ili aweza kufurahia huduma anayoipata. 
Kilahala alimaliza kwa kutoa wito kwa Taasisi za Umma na wadau waendelee
kuiamini TEMESA na kuendelea kufanya kazi na TEMESA na kuongeza kuwa
Wakala unakuja kivingine kuhakikisha wateja wanaridhishwa huku
akiwasihi wadau hao kulipa mkazo suala la ulipaji wa madeni ya huduma
wanazopatiwa kwani wakilipa  madeni yao, TEMESA itaweza kulipa wazabuni
kwa vipuri ambayo inawauzia ili wateja hao waridhishwe na huduma
wanazopatiwa.

About Author

Bongo News

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *