Wananchi wa Mkoa wa Manyara wameishukuru Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwapeleka wataalam wa afya mabingwa wa moyo kwa
ajili ya kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Hayo yamesemwa na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika Hospitali ya Rufaa
Mkoa wa Manyara (MRRH) kwa ajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya
siku tano iliyoanza leo ikifanywa na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkazi wa Babati vijijini Andrea Tluway alisema
ujio wa mabingwa kutoka JKCI kwake imekuwa fursa ya kuchunguza moyo wake
kwani hakuwahi kupimwa moyo na amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo
la damu.
“Niliposikia matangazo ya kambi hii sikupuuzia hii nafasi, tofauti na kuwa na shida
ya shinikizo la damu pia nimekuwa nikiona dalili tofauti tofauti katika mwili wangu
kama mapigo ya moyo kupiga kwa haraka, maumivu makali upande wa kushoto
wa kifua na moyo kuuma hivyo nikaona nivizuri leo nikapima moyo wangu
kufahamu kama nina shida ya moyo”, alisema Andrea
Aidha Andrea amewashauri wananchi wa mkoa wa Manyara na mikoa ya jirani
ambao bado hawajafika katika Hospitali hiyo kutumia nafasi hiyo yakipekee
ambayo Serikali ya awamu ya sita imewapa wananchi wa Manyara kufikiwa na
huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Agnes Hamad mkazi wa Manyara alisema miaka mitatu iliyopita alivimba sehemu
mbalimbali za mwili wake ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi ilionekana kuwa
upande mmoja wa moyo umejaa maji na kupatiwa dawa ambazo baada ya
kuzitumia na kurudi Hospitali aliona nafuu tofauti na alivyokuwa mwanzo.
Agnes anasema baada ya kusikia ujio wa Madaktari bingwa wa moyo wa JKCI
akaone ni wakati sasa kufanyiwa vipimo vya moyo na mabingwa hao ili aweze
kupata uhakika zaidi kama tatizo alilokuwa nalo mwanzo limeisha au anahitaji
matibabu zaidi.
“Naishukuru sana Serikali yetu kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kutuletea
wataalam karibu ili tuweze kutumia gharama kidogo kuchunguza afya zetu tofauti
na kama tungezifuata Dar es Salaam”, alisema Agnes
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Johnstone Kayandabila alisema JKCI imeweka utaratibu wa
kuwafuata wananchi mahali walipo kusogeza huduma karibu na wananchi
kuwasaidia wale ambao wasingeweza kupata nafasi ya kufuata huduma hizo JKCI
kupata huduma.
Dkt. Johnstone alisema wakazi wa Manyara wamejitokeza kwa wingi na tayari siku
ya kwanza wameshakutana na wagonjwa ambao wanahitaji kupewa rufaa
kwenda JKCI kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Kwa siku ya leo hadi mchana huu tumeshawapa rufaa watu wazima wawili
mmoja akiwa na maumivu ya kifua na mwingine mfumo wake wa umeme wa
moyo kuwa na hitilafu, pia watoto wawili ambao wana matundu kwenye moyo
tumewapa rufaa waweze kufika JKCI kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo”,
alisema Dkt. Johnstone
Naye kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) Dkt.
Yesiga Mutajwaa alisema Hospitali hiyo inatamani kuwe na muendelezo wa
ushirikiano baina ya JKCI na MRRH kwani MRRH bado ina changamoto katika
ufanyaji wa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram –
Echo)
Dkt. Yesiga alisema kupitia kambi hiyo wanaenda kuboresha mashirikiano kwani
MRRH ikipata wagonjwa hasa wale wanaohitaji upasuaji wa moyo huwa hawana
maamuzi nao zaidi ya kuwapa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa
moyo.
“Kwa wiki hii moja naamini wataalam wetu watapata nafasi ya kujifunza lakini pia
itatusaidia kufanya maamuzi kama tutawaomba JKCI warudi tena kwa ajli ya
kutufundisha au sisi tupeleke wataalam wetu JKCI kupata uzoefu”, alisema Dkt.
Yesiga